Na Florah Temba, Moshi-Kilimanjaro
Yetu
LICHA ya serikali
mkoani Kilimanjaro kulifunga bwawa la Nyumba ya mungu kwa kipindi cha miezi
sita kutokana na kupungua kwa kiasi kikubwa kwa uzalishaji wa samaki, hali
katika bwawa hilo bado imeelezewa kuwa mbaya kutokana na kuendelea kuwepo kwa
vitendo vya uvuvi haramu vinavyoendeshwa kwa wizi.
Bwawa hilo lililoko
wilayani Mwanga Mkoani Kilimajnjaro, lilifungwa Mwezi Februari mwaka huu, kwa
ushirikiano wa serikali ya mkoa wa Kilimanjaro na Manyara, kutokana na kupungua
kwa kina cha maji na kushamiri kwa uvuvi haramu.
Wakati Bwawa hilo
linafungwa samaki walikuwa wamepungua kutoka Tani zaidi ya 5,000 zilizokuwa
zikizalishwa kwa mwaka, hadi kufikia Tani 1770 kwa mwaka hali ambayo ilionekana
kuathiri sekta ya uvuvi.
Bwawa hilo ambalo
lilitakiwa kufunguliwa Septemba Mosi mwaka huu, bado halijafunguliwa na
linaelezewa kufunguliwa wakati wowote kuanzia sasa ingawa bado haijafahamika
kama samaki wameongezeka au la.
Akizungumza
mkuu wa wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Bw. Shaibu Ndemanga,
alikiri kuendelea kushamiri kwa vitendo vya uvuvi haramu katika Bwawa hilo,
licha ya kwamba bado halijafunguliwa.
Alisema pamoja na
Bwawa hilo kufungwa kwa nia njema ya kuacha samaki wawe wakubwa, bado vitendo
vya uvuvi haramu vilikuwa vikiendelea kwa wizi hali ambayo inaonekana kurudisha
nyuma jitihada za mkoa huo za kuinua sekta ya Uvuvi.
“Ni kweli bwawa hili
lilifungwa kwa miezi sita na lilitakiwa kufunguliwa tarehe moja mwezi wa tisa,
lakini bado halijafunguliwa na tutalifungua wakati wowote kuanzia sasa
,kwani yapo mambo ya Msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa ikiwa ni
pamoja na kuweka mikakati ya namna ya kulinda samaki”alisema
Hata hivyo mkuu huyo
alipoulizwa kama samaki wameongezeka alisema bado takwimu hazijatolewa na
kusisitiza kuwa pamoja na kufungwa kwa bwawa hilo wizi wa samaki ulikuwa
ukiendelea kwa kiasi kikubwa.
Akizungumzia suala la
ulinzi Bw. Ndemanga alisema ulinzi katika bwawa hilo unahitaji rasilimali
nyingi ikiwemo Mafuta kutokana na kwamba wavuvi huingia usiku kwa kificho na
kuendeleza uvuvi haramu jambo ambalo ni hatari kwa uzalishaji wa samaki.
Alisema wakati
bwawa hilo linafungwa yapo mambo mbalimbali ambayo yalitakiwa kutekelezwa kabla
halijafunguliwa ikiwa ni pamoja na vyombo vya uvuvi kusajiliwa,watu
kujisajili,kuundwa kwa vikundi na wananchi wa vijiji vinavyozunguka Bwawa
kuanzisha miradi mingine ya maendeleo ili kuondokana na hali ya kutegemea bwawa
hilo kama njia pekee ya kuwaingizia kipato.
Bwawa hilo linatumiwa
na wilaya Tatu ikiwemo wilaya ya Mwanga ambayo inawavuvi zaidi ya 3.000 na
ambao wameshajisajili hadi sasa ni wavuvi 600 pekee.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment