Na Florah Temba, Moshi-Kilimanjaro Yetu
CHAMA cha mapinduzi
(CCM) mkoani Kilimanjaro, kimewataka wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi
ndani ya Chama hicho, kuacha kuwarubuni wanachama kwa kuwapa rushwa ili
wawachague, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume cha taratibu na kutasababisha
kupatikana kwa viongozi wasio waadilifu.
Rai hiyo imetolewa na
katibu wa chama hicho mkoani Kilimanjaro Bw. Steven Kazidi, wakati akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mchakato wa uchaguzi ndani ya
chama hicho mkoani humo.
Bw. Kazidi alisema chama
hicho hakitavifumbia macho vitendo vya rushwa katika uchaguzi, na kwamba
mgombea yeyote atakayebainika kushinda kwa kutoa rushwa, ataadhibiwa kwa kanuni
za chama ikiwemo kunyang’anywa ushindi wake ili kuweza kuwa fudisho kwa watu
wengine wenye tabia kama hizo.
“Nitoe wito kwa
wagombea wote katika mkoa huu, waache kutoa rushwa ili wachaguliwe, kwani hali
hiyo ni kinyume cha taratibu za chama na hatutavifumbia macho vitendo hivyo”
alisema Kazid.
Aidha Bw. Kazidi
aliwataka pia wanachama wa chama hicho kuwachagua viongozi ambao ni
waadilifu,waaminifu na wachapakazi ambao watakijenga chama na si
kukibomoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanawaepuka viongozi wanaohitaji madaraka
kwa vigezo vya rushwa.
Alisema viongozi
wanaotaka kununua uongozi kwa rushwa hawafai kutokana na kwamba uongozi
haununuliwi hivyo ni vema wanachama wakawaepuka na kuhakikisha hawawachagui.
Katika mkoa wa
Kilimanjaro uchaguzi ulianza jana Octoba Tatu katika wilaya ya
Same,Mwanga na Rombo,ambapo katika wilaya ya Mwanga Mathew Msofe ametetea
kiti chake cha uenyekiti kwa kupata kura 527, huku kiti cha NEC
kikichukuliwa na Anania Tadayo ambaye aligombea ubunge mwaka 2010 na
kupata kura 41.
Uchaguzi huo
unaendelea leo Octoba 4, wilaya ya Hai, Octoba Tano Moshi mjini, na octoba 12
utafanyika katika wilaya ya Siha na Moshi Vijijini.
Ngazi ya mkoa
uchaguzi huo utafanyika Octoba 15 ambapo utamchagua mwenyekiti wa Mkoa na
wajumbe wa halmashauri kuu ya mkoa ambapo wagomnbea wa nafasi ya mwenyekiti ni
Mildred Kisamo,James Kombe,Idd Juma na Thomas Ngawaiya.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment