Na Upendo Mosha, Moshi Vijijini
WAKUU wa Idara katika Halmashauri ya Wilaya ya
Moshi Vijijini, wametakiwa kuacha mara moja tabia ya kuhodhi mafuta ya magari
na kuacha kuzigeuza ofisi hizo kama mali yao.
Hayo yalibainishwa jana na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Moris Makoi wakati
wa kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri
hiyo.
Makoi alisema, wakuu wa idara mbalimbali katika halmashauri hiyo, wamekuwa
wakijisahau katika utendaji kazi na kukiuka kanuni za kazi zao.
Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wakuu wa idara, kuhodhi mafuta ya magari
na kuyafanya kama mali yao pasipo kufahamu kuwa, magari hayo ni mali ya
halmashauri hiyo na yapo chini ya mkurugenzi wa halmashauri.
“Tatizo la hii halmashauri kila mtu anajifanya yeye ni mkurugenzi, kumekuwa na
tabia ambayo haipendezi hasa kwa watu wasomi kama nyie kuhodhi mafuta ya
magari.
“Jambo hili si zuri ni kinyume na taratibu za kazi za halmashauri, nataka tabia
hiyo iachwe mara moja kabla ya hatua nyingine za kinidhamu kuchukuliwa,”
alisema Makoi.
Alisema watumishi hao wamekuwa wakijisahau kuwa ofisi hizo ni za wananchi na
kuzifanya kuwa mali zao pasipo kutekeleza yale ambayo yapo katika misingi ya
kazi zao.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Edwini Siyae, alikiri
kuwapo kwa tatizo hilo na kusema kuwa, halmashauri hiyo inakabiliwa na matatizo
mengi.
Alisema kumekuwa na tatizo hilo la kuhodhi mafuta mara kwa mara, jambo ambalo
limekuwa likikwamisha juhudi za maendeleo katika halmashauri hiyo.
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment