Na Upendo Mosha, Hai
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Kilimanjaro,
linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuhujumu miundombinu ya umeme, jambo
ambalo ni hatari kwa maisha ya watu na linaloweza kusababisha vifo.
Akizungumzia tukio hilo la kukamatwa kwa watu hao, Meneja wa TANESCO wilayani
Hai, James Chinula, alisema kukamatwa kwa watu hao kumetokana na msako mkali
uliofanywa katika wilaya hiyo katika vijiji vya Machame, Masama na Hai mjini.
Alisema watu hao walikamatwa baada ya kugundulika kujiunganishia umeme isivyo
halali kwa kupitisha waya katika nguzo na kisha kuchimbia chini ya ambao ambapo
waya hizo zimechubuka, jambo ambalo alisema ni hatari kwa maisha ya watu.
Aliwataja watu hao kuwa ni Ally Omary, Stephano Eliafiye, Yohana Zacharia,
Arnold Jonas, Shani Ulomi pamoja na Sharifa Ally, wote wakazi wa Hai.
Vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme vimekuwa vikishamiri mkoani hapa na
kwamba baadhi ya watu pia wamekuwa wakichangia ukatikaji wa umeme mara kwa mara
na kusababisha shirika hilo kutupiwa lawama.
“Operesheni hii tumefanikiwa kukamata watu saba na hii ni muendeleo wa msako
unaofanywa nchi nzima na wilaya yetu ni miongoni mwa wilaya zenye changamoto ya
tatizo hili jambo ambalo limekuwa likitusumbua sana katika utoaji wa huduma
zetu,” alisema.
Chinula aliwataka wananchi kushirikiana na shirika hilo kufichua uhalifu wa
wizi wa umeme na kwamba kufanya hivyo kutapunguza matukio ya vifo na ukatikaji
wa umeme wa mara kwa mara wilayani hapa
Chanzo: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment