na Rodrick Mushi, Rombo
TATIZO
la mfumo dume kwa baadhi ya wazazi wilayani hapa limeelezwa kupungua, hususani
katika kutoa fursa sawa katika kuwapatia watoto wa kike na wa kiume elimu
pamoja na kurithi mali.
Kipindi
cha nyuma Rombo ilikuwa miongoni mwa wilaya zilizokuwa zikikabiliwa kwa kiwango
kikubwa na mfumo dume, ikiwemo watoto wa kike kutokuwa na haki ya kumiliki
ardhi pamoja na elimu.
Mkuu
wa Shule ya Sekondari Shauritanga iliyopo wilayani hapa, inayomilikiwa na
Jumuiya ya Wazazi wa CCM, Kalisti Shirima, akizungumza kwenye mahafali ya
kidato cha nne, alisema kuwa tatizo hilo lilichangiwa na umaskini kwa kiwango
kikubwa.
“Mfumo
dume kipindi cha nyuma ulikuwa unasumbua maana nilikuwa napata matatizo hayo
kwa wanafunzi wa kike ambao wazazi wao walikuwa hawataki kuwalipia ada, lakini
baada ya wananchi wengi kuwa na uwezo wa kifedha, tatizo hilo limepungua,”
alisema.
Pamoja
na umaskini, alisema pia hatua ya wananchi kuelimika pamoja na kujua umuhimu wa
kutoa elimu kwa watoto wote na kuwarithisha mali bila kubagua imesaidia.
Kwa
upande wake Kaimu Katibu tawala wilayani Rombo, Yusuph Kasuka, aliyekuwa mgeni
rasmi kwenye mahafali hayo, alisema kuwa jamii inatakiwa kuondokana na vitendo
hivyo vya ubaguzi wa kijinsia.
Alisema
kuwa sera ya elimu inaeleza kuwa mwanafunzi ambaye ana umri wa kuanza shule
anatakiwa kuwepo shuleni, lakini wazazi ambao wamekuwa wakikiuka sheria hiyo ni
vyema wakapewa elimu, na kama wanakiuka basi sheria zichukue mkondo wake.
Kasuka
alisema sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo elimu
ya vitendo ambapo jitihada zaidi zinahitajika kwa wadau na serikali kuweza
kumudu ushindani wa soko la pamoja la Afrika Mashariki.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment