Bi Levina Swai enzi ya uhai wake
Rombo. Ilikuwa ni majonzi, vilio na huzuni katika kijiji cha Mahalu,
wilayani Rombo, Kilimanjaro kufuatia mazishi ya aliyetarajiwa kufunga
ndoa Jumamosi marehemu Levina Swai pamoja na mwanawe.
Marehemu Levina alizikwa na mwanaye kaburi moja baada ya kichanga hicho
kufariki siku hiyo hiyo mara baada ya mama yake kupoteza maisha kwa kile
kilichodaiwa ni kuugua Malaria, shinikizo la damu kuwa chini na
upungufu wa damu.
Marehemu Levina alifariki wilayani Handeni, mkoani Tanga.
Akizungumza katika kijiji cha Mahalu kata ya Makiidiwilayani Rombo,
alikozikwa,wifi wa marehemu, Hortensia Mrima alisema wifi yake alifia
hospitalini na alikuwa mwalimu wa Shule ya Msingi Nndawa mkoani Lindi
akiwa katika mpango wa ajira ya walimu wapya.
“Mimi ndiye nilikuwa namuuguuza hospitalini tangu Alhamisi iliyopita na
alikuwa anasumbuliwa na malaria na kupungukiwa na damu na pressure
(shinikizo la damu) kuwa chini,”alisema Mrima.
Ibada ya mazishi ilianza saa 8:30 mchana ikiongozwa na Padri Emmanuel
Mavengero na kuhudhuriwa na waombolezaji kutoka Tanga na Kilimanjaro.
Mazishi hayo yalitawaliwa na simanzi huku waombolezaji wengi akiwamo
aliyetarajiwa kumuoa marehemu Levina,Gabriel Swai muda wote alikuwa
akibubujikwa na machozi na kushindwa kuzungumza.
Wifi huyo alieleza kuwa wifi yake alipopimwa alikutwa na Malaria 13 na
kupewa dawa za malaria za SP na dripu za Quinine ambazo zilimlewesha
sana na kuendelea kudhoofu.
“Siku hiyo ya Alhamisi alikata kauli akawa haongei ikabidi daktari
amwekee dripu za Glucose ili kumuongezea nguvu na shinikizo la damu
ilirudi sawasawa lakini bado alikuwa amelegea na alikuwa
haongei,”alisema.
Ilipofika Jumamosi ambayo ndiyo siku iliyokuwa imepangwa kufunga ndoa na
Gabriel Swai, ikabidi madaktari wamuwekee maji ya uchungu ili kumuokoa
mtoto baada ya mama kuwa mahututi.
“Yale maji ya uchungu yalimsaidia akaweza kujifungua mtoto wa kiume
mwenye uzito wa kilo 1.7 na baada ya kujifungua alipoteza fahamu na saa
8:05 mchana akafariki dunia,”alisema.
Kwa mujibu wa Mrima, mtoto aliendelea kuishi huku akipewa maziwa lakini
alikuwa akiyatapika, hadi ilipofika saa 5:00 usiku alifariki dunia
“Huwa tunasikia mtu anakufa baada ya kufunga ndoa lakini hili la wifi
yetu kuwa siku ambayo ndiyo walipanga kufunga ndoa na kaka yetu
limetushtua sana,”alisema dada huyo wa aliyetarajiwa kufuga ndoa na
marehemu.
Baba mzazi wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja tu, Mmasi
aliwaomba waombolezaji kumuomba Mungu na kujiandaa kwani hawajui siku
wala saa watakayotwaliwa.
Akizungumza katika mahubiri ya ibada hiyo, Padre Mavengero, alikemea chuki za kidini zinazoanza kupenyezwa nchini.
“Watu waishi vizuri kwa amani na wapendane waache kuchochea mfarakano wa
kidini… Waislamu na Wakristo ni marafiki na ndiyo maana tumeshirikiana
tangu Handeni hadi Rombo,”alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya harusi,Abdi Kipacha ambayo baadaye kamati yake
ilijigeuza kuwa ya msiba, alikabidhi kwa mfiwa Sh500,000 zilizokuwa
zimetengwa kwa zawadi kwa ajili ya maharusi ambazo jana zilikabidhiwa
kama rambirambi.Msiba huo umekuwa gumzo nchini hasa baada ya gazeti hili
kuripoti tukio hilo lililotokea Handeni mkoani Tanga ambalo si la
kawaida
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment