Home » » Moto wateketeza Mlima Kilimanjaro

Moto wateketeza Mlima Kilimanjaro

 Fadhili Athumani na Safina Sarwatt, Kilimanjaro
MOTO umezuka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) na kuteketeza zaidi ya ekari 40 za mlima huo. Moto huo ulianzia katika Wilaya ya Rombo, maeneo ya Amboni, Ushiri, Keryo, Kimori na Shimbi, kabla ya kuenea na kusababisha hasara ambayo hadi sasa bado haijafahamika.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mkuu wa Idara ya Uhusiano na Mawasialiano wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Paschal Shelutete, alisema moto huo ulizuka juzi mchana.

Katika taarifa hiyo, Shelutete alisema kuwa, taarifa za awali zinaonyesha chanzo cha moto huo ni uvunaji haramu wa asali katika eneo la Amboni, ambapo watu waliingia ndani ya hifadhi na kuvuna asali kwa kutumia moto. Baada ya moto huo kusambaa na kuwashinda kuzima, watu hao walikimbia.

Kwa mujibu wa Shelutete, inakadiriwa eneo lililoteketezwa kwa moto linakadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari 40.

Alisema kwamba, hatua zilizochukuliwa na TANAPA hadi sasa ni kuwashirikisha wananchi wa maeneo jirani ya Mshiri, Lyasongoro, Amboni, Ushiri na Ikuwini, waliokuwa katika maeneo ya jirani na eneo la tukio ili kukabiliana na moto huo.

Pamoja na hayo, alisema wanafunzi kutoka katika Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU), walitumwa kuelekea eneo la hifadhi lililoathiriwa na moto huo kusaidia jitihada za kuuzima.

CHANZO GAZETI LA MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa