Na Florah Temba,
Rombo.
WANAFUNZI 30 kutoka shule mbalimbali za sekondari katika wilaya ya
Rombo mkoani Kilimanjaro, walishindwa kuendelea na masomo katika kipindi cha
mwaka 2012, kutokana na kupata ujauzito.
Wanafunzi hao wa Kike ambao walikatisha masomo wengi wao wanaelezewa
kuwa walikuwa kidato cha nne, hivyo kujikuta wakitia doa ndoto zao kutokana na
kutoendelea na masomo.
Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari ofisini kwake Afisa
Elimu ya sekondari katika wilaya ya Rombo Bw. Juma Kinanda, alisema kati ya
wanafunzi hao 30 wanafunzi 28 ni kutoka shule za sekondari za serikali na
wawili kutoka shule za binafsi.
Bw. Kinanda alisema tatizo la mimba mashuleni bado ni tatizo ambalo limekuwa likisababisha baadhi
ya watoto wa kike kukatisha masomo, na hivyo kujikuta wakiishia kuishi maisha
ya mitaani baada ya ndoto zao kuzimika.
Aidha alisema tatizo hilo limekuwa likichangiwa kuwa kubwa na baadhi
ya wazazi kutoshtushwa na hali hiyo na kuona ni jambo la kawaida huku wengine
wakidiriki kukataa kutoa ushirikiano pindi watoto wao wanapobainika kupata
ujauzito.
“Tatizo hili la mimba mashuleni liko kwa aina mbili, moja ni
wanafunzi wanaopata ujauzito kugoma kuwataja wahusika ili sheria ichukue mkondo
wake kukomesha tatizo, lakini pili ni wazazi kukataa kutoa ushirikiano kwa
wakuu wa shule pindi watoto wao wanapopata ujauzito,kwa kweli hili ni tatizo ambalo linachangia tatizo
kuendelea kuwa kubwa”alisema Bw. Kinanda.
Alisema wapo baadhi ya wazazi katika wilaya ya Rombo, ambao hudiriki
kuwatorosha watoto wao manyumbani kupoteza ushahidi,mara baada ya kugundulika
kupata ujauzito wakiwa shuleni,ili kukwamisha jitihada za wakuu wa shule husika
za kufuatilia wahusika kwa lengo la kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa
dhidi yao.
“Wazazi wamekuwa tatizo kubwa katika kudhibiti suala hili la mimba
mashuleni kwani pamoja na kukataa kutoa uishirikiano, pia wamekuwa
wakiwatorosha watoto wao nyumbani mara baada ya kugundua kuwa amepata ujauzito
na mkuu wa shule anafuatilia ili kumjua muhusika na kumfikisha katika vyombo
vya sheria,na hili linawafanya wahusika kuendeleza vitendo hivyo kutokana na
kutochukuliwa hatua zozote”alisema.
Alisema kukosekana kwa mabweni
kumekuwa pia chanzo cha
mimba mashuleni kutokana na kwamba wanafuzni wengi huishi katika nyumba za
kupanga(Geto) na hivyo kujikuta wakijihusisha na masuala ya kimapenzi kutokana
na kukosa uangalizi wa wazazi au walimu.
0 comments:
Post a Comment