Home »
» Hali mpakani na Holili bado tete
Hali mpakani na Holili bado tete
|
|
HALI bado si shwari katika mpaka wa Tanzania na Kenya katika
kituo cha Forodha cha Holili, baada ya wafanyabiashara wa Tanzania
kupinga hatua ya serikali ya Mkoa wa Kilimanjaro kushinikiza kufutwa
vibali vyao vya kusafirisha mazao kwenda nchini Kenya.
Novemba mosi mwaka huu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilifuta
vibali vya wafanyabiashara wa Tanzania kusafirisha mazao ya nafaka
kwenda nchini Kenya lakini Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa,
iliiteua Kampuni ya Kilimanjaro Uchumi kuchukua jukumu hilo, hatua
ambayo ilipingwa vikali na wafanyabiashara hao.
Kutokana na hali hiyo, juzi na jana hali haikuwa nzuri katika mpaka
huo kutokana na tishio la wafanyabiashara wa Tanzania kutaka kuzuia
magari ya Kenya yasiingie nchini kupakia mazao ya nafaka.
Juzi magari sita yaliyokuwa yamesheheni mazao ya nafaka yakiwa na
namba za usajili za nchini Kenya, yalizuiliwa upande wa Tanzania kwa
saa sita na polisi wenye silaha kutokana na agizo la Kamati ya Ulinzi
na Usalama kuwazuia wafanyabiashara wasipeleke mazao hayo nchini Kenya.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika kituo hicho cha Forodha
cha Holili, wafanyabiashara hao wamemshutumu Mkuu wa Mkoa wa
Kilimanjaro, Leonidas Gama, kwa madai ya kuibeba kampuni hiyo.
Wafanyabiashara hao wamelalamika kuwa uamuzi huo utawaumiza na
wanaweza wakajikuta kwenye wakati mgumu na vyombo vya fedha kutokana na
kushindwa kurejesha mikopo waliyopata benki.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Gama, jana alipuuza
shutuma hizo na kudai kuwa kuna watu wachache ambao hawataki kufuata
taratibu zilizowekwa na kwamba wachache hao wana sababu zao binafsi.
Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa alisema kampuni hiyo imeteuliwa na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kwa lengo la kukusanya mapato katika
mpaka huo na kudhibiti mianya ya ufujaji wa mapato.
Mwezi Septemba na Oktoba mwaka huu Wizara ya Kilimo, Chakula na
Ushirika ilitoa kibali kwa kampuni za Kisongo Grain Market, Osaka
Stores na Abdilah Mkilindi kusafirisha mazao ya nafaka kwenda nchini
Kenya, kibali ambacho muda wake ulikuwa umalizike Desemba 30, mwaka
huu.
Chanzo;Tanzania Daima
|
|
1 comments:
Wafanyabiashara kwa ajili ya masoko ya EAC,SADC,COMESA,AGOA,nk wanakaribishwa kujiunga Tanzania Exporters Association (TANEXA) kwa ajili ya
kujenga nguvu ya pamoja ili kupata uwezeshaji wa kukabiliana na changamoto zinazoizunguka sekta hii muhimu kiuchumi
Email:info@tanexa.com
www.tanexa.com
Blogu:tanexa.blogspot.com
Post a Comment