SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) kwa kushirikiana na Jeshi la
Polisi, limeendesha operesheni maalumu katika masoko makubwa ya nguo za
mitumba katika miji ya Moshi na Arusha yanayodaiwa kuwa wauzaji wakuu
wa nguo za ndani zilizopigwa marufuku.
Operesheni hiyo iliyoanza katika masoko ya Klolotoni na soko la Kati
na Unga Limited ya jijini Arusha, ilifanyika pia juzi katika masoko ya
Meimoria na Mbuyuni ambapo robota zaidi ya tano zilikamatwa na kisha
kuteketezwa katika dampo la Kaloleni.
Ofisa Viwango na Mkaguzi mwandamizi wa shirika hilo, Paul Manyilika
akizungumza muda mfupi baada ya kuihitimisha zoezi hilo mjini hapa,
alisema zoezi hilo litakuwa endelevu kutokana na baadhi ya
wafanyabiashara kukaidi agizo la serikali.
“Nguo hizo zina madhara kwa afya ya binadamu na bahati mbaya wengi
wetu tunashindwa kutafsiri nini maana ya nguo ya ndani. Nguo ya ndani
ni pamoja na chupi, sidiria na soksi na nguo za kulalia ambazo kwa
ujumla wake zote hizi zimepigwa marufuku,” alisema Manyilika.
Alisema marobota ya nguo hizo yaliyonaswa na TBS katika operesheni ya
kushtukiza iliyofanyika mjini Moshi yameteketezwa na maofisa wake
chini ya ulinzi wa polisi na kwamba wahusika hao kwa sasa wanafanyiwa
mahojiano, ili kubaini watu hao wanaingizaje nguo hizo.
“Nguo hizi zinasambaza magonjwa ya kitropiki (Tropical Diseases) na
kiwango kikubwa cha Watanzania wameathiriwa hasa na magonjwa ya ngozi,”
alisema Manyilika.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment