WATALII wanane raia wa Australia waliokuwa nchini kwa ajili ya
kupanda mlima Kilimanjaro na kutembelea vivutio vya utalii katika
visiwa vya Zanzibar, wamejikuta katika wakati mgumu baada ya kutapeliwa
zaidi ya dola 7,000 za Kimarekani sawa na sh milioni 10.5 za
Kitanzania na kampuni moja ya utalii mjini hapa.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa kiasi hicho cha
fedha kinajumuisha gharama za kupanda mlima Kilimanjaro, chakula na
malazi kwa siku tatu na kutembelea vivutio vya utalii katika visiwa vya
Zanzibar kwa siku tatu.
Tukio hilo limetokea Januari 9, mwaka huu baada ya wageni hao kupanda
mlima Kilimanjaro kupitia lango la Machame, lakini baada ya kuteremka
mlimani Januari 15, watalii hao walizuiliwa na maofisa wa Hifadhi ya
Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) katika lango la Mweka wakidaiwa
malipo ya siku tano.
Pamoja na watalii hao kujitetea kuwa walikuwa tayari wameshalipa
gharama zote za kupanda mlima huo kwa siku saba, bado maofisa wa KINAPA
waliendelea kuwashikilia hadi hapo walipofanya mawasiliano na wenzao
Australia na kutumiwa fedha na hatimaye kulipa dola 4,800 sawa na sh
7,680,000 kutokana na kampuni hiyo kulipa malipo ya siku mbili tu.
Wakati hali ikiwa hivyo, Mkurugenzi wa Kampuni hiyo (jina
limehifadiwa), kwa muda wa wiki mbili sasa amekuwa hapatikani ofisini
kwake tangu kutokea kwa tukio hilo na simu zake zote za kijangani
zimekuwa zikizimwa muda wote huku akimtumia mtu mmoja aliyejitambulisha
kwa jina moja (tunalo) kumsemea.
Kutokana na tukio hilo, watalii hao walilazimika kufuta safari yao ya
kutembelea vivutio vya utalii visiwani Zanzibar kutokana na mwenyeji
wao kuingia mitini huku wapagazi wakishikilia vifaa vya kupandia mlima
huo kutokana na kampuni hiyo kutowalipa mishahara yao.
Mbali na watalii hao, watalii wengine saba raia wa Sweden, nao
wamejikuta wakionja joto ya jiwe baada ya kushilikiwa kwa zaidi ya saa
kumi katika lango la Mweka baada ya kudaiwa malipo ya siku moja
kutokana na kampuni iliyowapandisha mlima huo kulipa malipo ya siku
sita badala ya saba.
Watalii hao walipanda mlima Kilimanjaro Januari 4 kupitia lango la
Machame na kushuka Januari 10 kupitia kwa mfanyabiashara mmoja Filbert
Laswai aliyenunua vocha kutoka Kampuni ya Kili Boy’s na kupewa kibali
namba 125219.
Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, Laswai alikiri
kutokea kwa tukio hilo huku akijitetea kuwa tatizo hilo lilitokana na
mshirika wake kibiashara raia wa Kenya ambaye hakumtaja jina
kuchelewesha malipo.
Mfanyabiashra huyo ambaye ni mtoto wa mfanyabiashara maarufu mjini
hapa, Epmark Laswai, pia alikiri kudaiwa vifaa vya kupandia mlima na
kampuni ya ukodishaji vifaa ya ASCEND Tanzania vyenye thamani ya sh
662,000.
Wapagazi waliotumika kubeba mizigo ya watalii hao vikiwamo vyakula,
nao wameshikilia vifaa vya kampuni hiyo wakidai mishahara yao
inayokadiriwa kufikia sh 2,755,000.
Hata hiyo meneja uhusiano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA),
Pascal Shelutete, kwa wiki mzima amekuwa hatoi ufafanuzi juu ya matukio
ya watalii kutapeliwa na kampuni hizo licha ya mwandishi wa habari
hizi kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi mara kwa mara bila mafanikio.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya ASCEND Tanzania
inayojihusisha na ukodishaji wa vifaa vya mlimani, Fred Namwandu,
amedai kupata hasara kubwa kutokana na vifaa vyake kushikiliwa na
wapagazi kwa zaidi ya wiki tatu sasa huku pia kampuni hizo zikishindwa
kumlipa fedha zake.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment