Gari binafsi la Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania
(TCB), Injinia Adolf Kumburu lililoibwa na watu wasiojulikana mjini
Moshi, Oktoba mwaka jana, limekamatwa jijini Dar es Salaam.
Habari za uhakika zilizothibitishwa na polisi,
zilisema gari hilo aina ya Toyota Raum lilikamatwa na polisi, baada ya
kulitafuta kwa miezi mitano mfululizo.
Gari hilo lililoibwa mjini Moshi Oktoba 4, 2013
lilikamatwa wiki iliyopita na limehifadhiwa katika Kituo cha Polisi cha
Kawe cha jijini Dar es Salaam na watuhumiwa kadhaa nao wanashikiliwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
jana alithibitisha kukamatwa kwa gari hilo, kulikowezeshwa na kuwapo
kwa taarifa za kiintelijensia za polisi na ushirikiano wa raia wema.
“Ni kweli Polisi tumefanikiwa kulikamata gari hilo
likiwa limebandikwa nambari bandia na tayari mke wa Kumburu (hakumtaja
kwa jina) ameshalitambua gari hilo pale Kawe,” alisema Boaz.
Katika wizi huo uliotokea kati ya saa 6:00 na saa
7:00 mchana nyumbani kwa mkurugenzi huyo eneo la Shanty Town mjini
Moshi, vitu vingine vyenye thamani ya mamilioni ya shilingi pia
viliibwa.
Kumburu aliwahi kukaririwa na gazeti hili mwaka
jana akitaja vitu vingine kuwa ni runinga aina ya Samsung Flat Screen
inchi 36, Deck aina ya Phillips, Micro-Wave, kompyuta mpakato aina ya
Apple Mac Book, Samsung Min-Tablet na Digital kamera mbili.
Pia wezi hao waliiba simu mbalimbali za familia
zipatazo nne moja ikiwa ni Blackberry na tatu aina ya Nokia na redio
ndogo inayoshika masafa ya kimataifa, begi kubwa la nguo na jozi za
viatu.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment