UONGOZI wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA)
umeahidi kuongeza jitihada za kupigana dhidi ya usafishaji wa dawa za
kulevya kutokana na maboresho yaliyofanyika katika kitengo cha usalama
cha uwanja huo.
Tamko hili limekuja siku chache baada ya Mtanzania, Mastura
Makongoro, mwenye hati ya kusafiria namba AB26695 kukamatwa na dawa za
kulevya zinazodhaniwa kuwa ni cocaine, zenye uzito wa kilogramu 4.8,
akielekea Ghana.
Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Fedha na Huduma za
Kibiashara wa Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO), Bakari
Murusuri, ilieleza uwanja huo umejizatiti kupigana na usafarishaji wa
dawa za kulevya kupitia uwanja huo.
Murusuri alisema maofisa usalama wa uwanja huo, Jumanne usiku wa
manane walimkamata mwanamke huyo wakati akisubiri kupanda ndege ya
Shirika la Ethiopia kuelekea mjini Addis Ababa.
Alisema wakati wa uchunguzi, mwanamke huyo alitubu kuwa aliambatana
na mwenzake raia wa Nigeria, Mike Nwankwo (41), ambaye alimsindikiza
mpaka uwanjani na alikuwa ni miongoni mwa mtandao wa wasafirishaji wa
dawa hizo.
“Jeshi la Polisi na walinzi wa usalama hapa uwanjani waliunganisha
nguvu ili kumsaka mtu huyo na baadaye alikutwa kwenye maegesho ya
magari akisubiri kuhakikisha mwanamke huyo ameondoka nchini,”
aliongeza.
Murusuri alisema tangu Machi mwaka jana mpaka sasa uwanja huo wa
ndege umefanikiwa kukamata watu tisa wakihusishwa na usafirishaji wa
dawa za kulevya na kuahidi kuwa uwanja huo umejizatiti kikamilifu
kukabiliana na suala hilo.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment