Home » » Mvua:Majanga Same, Mwanga

Mvua:Majanga Same, Mwanga


Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga
 
Mvua zilizonyesha katika Wilaya za Mwanga na Same mkoani Kilimanjaro, zimesababisha maafa makubwa, huku mtu mmoja akiripotiwa kufa na wengine 980 wa kaya 196 wakipoteza makazi.
 Mvua hizo zimeelezewa kusababisha watu wengine 855 wa kaya 171 kuachwa bila vyakula baada ya kusombwa na mafuriko na kujikuta wakilazimika kuishi kwa kula mlo mmoja kwa siku ili kunusuru maisha yao.

Nao wanafunzi zaidi ya 300 wa Shule ya Msingi Mangiyo, iliyopo Ugweno wilayani Mwanga wamekatisha masomo kwa muda usiojulikana kutokana na vyumba vitano vya madarasa na ofisi ya walimu kuharibiwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua hizo.

Mtu huyo ambaye bado hajafahamika, alikutwa na umauti kufuatia mvua zilizonyesha kwenye safu za milima ya Upare wilayani Same kwa siku nne mfululizo .

 Kaya hizo  171 zinazoishi kwa mlo mmoja wilayani humo, zimepokea msaada na mahitaji mengine ya kibinadamu kutoka kwa wasamaria wema.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga, aliliambia NIPASHE kuwa hadi kufika jana asubuhi zaidi ya kaya 25 zilikuwa hazina makazi wala chakula kutokana na nyumba zao kubomolewa na vyakula kusombwa na maji.

“Shule ya Mangiyo kule Ugweno imeharibiwa vibaya na mvua zinazoendelea kunyesha.

Wanafunzi wamerejea majumbani kwa sababu hawana madarasa matano wala ofisi ya walimu,” alisema Ndemanga.

Aliongeza: " Lakini pia kuna kaya 25 hazina makazi wala chakula...Mimi na kamati yangu ya ulinzi na usalama tumeanza kufanya tathmini ya hali ya uharibifu wa mali ili kuona tutafanya nini kama serikali.”

Hali kama hiyo pia, imeiathiri Wilaya ya Same kutokana na mvua hizo zilizonyesha kwa siku nne sasa.

Mtu huyo kutoka jamii ya wafugaji katika mji mdogo wa Hedaru alikufa maji baada ya kujaribu kujiokoa wakati aliposombwa na mafiriko  yaliyokuwa yakishuka kwa kasi katika safu za milima ya Upare.

Mkuu wa Wilaya hiyo ya Same, Herman Kapufi, aliliambia NIPASHE jana kwa njia ya simu kwamba, mbali na kusababisha kifo hicho, pia kaya 171 hazina makazi wala chakula licha ya usalama wao kuwa shakani kutokana na kulala nje.

“Tumeokota maiti ya mtu mmoja (hajatambuliwa jina lake) aliyekuwa akichunga ng’ombe kule Hedaru, ambaye hata hivyo, alifariki wakati akijiokoa asisombwe na maji,” alisema Kapufi.

Aliongeza: “Mwili wake umehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Same ukingoja kutambuliwa na ndugu. Nawaomba wananchi wajitokeze hospitalini ili atambuliwe na kwenda kuzikwa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu.”

Alisema kufuatia hali hiyo, Shirika la World Vision limetoa msaada wa tani 148 za mahindi kwa ajili ya kuokoa maisha ya waathirika wa mvua hizo, ambazo kila mwananchi aliyeathirika atagawiwa kilo 25 za unga kwa ajili ya kujisitiri na njaa.

Wakati maafa hayo yanatokea, Serikali ya Wilaya hiyo tayari ilikuwa imeomba msaada wa chakula kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa na ikapokea juzi tani 897 za chakula kutoka Ghala la Taifa la Chakula (NRFA) kwa ajili ya kugawa katika vijiji vilivyokumbwa na njaa.

Alivitaja vijiji vilivyoathirika zaidi na mvua hizo kuwa ni Makanya yenye kaya 118, Saweni 25, Kasapo 19 na Hedaru tisa.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa