Home » » WAGOMA KUUZA NYAMA KWA SIKU MBILI

WAGOMA KUUZA NYAMA KWA SIKU MBILI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 



Baadhi ya mabucha yaliyofungwa.

Wauzaji wa Nyama wakiwa nje ya mabucha yao baada ya kugoma kuuza nyama.
Baadhi ya mabucha yaliyofungwa.
Na Dixon Busagaga wa 
Globu ya Jamii, Moshi

WAKAZI wa mji Manispaa ya Moshi, wametaabika kwa siku mbili sasa wakiwa hawapati kitoweo cha Nyama baada ya halmashauri ya manispaa hiyo na mamlaka ya udhibiti wa Chakula na dawa TFDA kuyafunga maduka ya nyama ambayo hayakidhi vigezo vya afya.

Katika hali inayoonesha kuwapo kwa mgomo wa wauza nyama,pamoja na manispaa kuyafunga maduka sita tu ambayo yalibainika kutokidhi vigezo, katika manispaa hiyo yenye maduka zaidi ya 50, lakini hakuna hata moja linaloendelea na biashara hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wenzake, Damian Temba alisema pamoja na kwamba manispaa ilitoa muda wa wafanyabiashara kuyafanyia marekebisho maduka yao lakini bado masharti waliyoweka hayatekelezeki.

"Tulipewa notisi yenye masharti 16, ikiwamo bucha kuwa na kiyoyozi, msumeno maalum wa kukata nyama, kuwapo kwa vioo na leseni ya TFDA.......hii misumeno haipatikani na iliyopo haina ubora na bei yake ni Zaidi ya Mil 1 ambayo ni vigumu kuinunua"alisema.

Alisema maduka mengi yamefanyiwa ukarabati uliohitajika lakini baadhi yao walilipa fedha ili kupata kibali cha TFDA lakini bado hawajaletewa jambo ambalo limeendelea kukwamisha jitihada zao za kutimiza masharti yaliyowekwa.

Hata hivyo wafanyabiashara hao walisema wakati manispaa ikifunga maduka yao, hali ni tofauti katika machinjio yanayomilikiwa na manispaa hiyo ambayo walidai ni machafu na hayakidhi vigezo vilivyowekwa na TFDA.

"Manispaa haitutendei haki hata kidogo, machinjio ni machafu mno, yanahatarisha afya za walaji,lakini hawaangalii hilo,wanatubana na maduka yetu ambayo tayari yamekamilika na kilichokosekana ni misumeno ambayo hata hivyo nayo haina ubora"alisema.

Alisema waliagizwa kwenda kujifunza maduka ya mfano mkoani Dodoma lakini pamoja na kuyaona hayatofautiani na waliyonayo jambo linalowatia shaka kama haki inatendeka au la.

Kwa mujibu wa notisi ya manispaa hiyo ya Novemba 20, 2013 yenye kumbukumbu namba MMC HO/7012/Vol III/132 na kusainiwa na afisa afya wa manispaa hiyo V.M Makundi lilitaja wahudumu kuvaa sare,kupimwa afya kila miezi 6 na yapigwe rangi nyeupe ndani.

Masharti mengine ni pamoja na chumba cha duka kiwe na ukubwa wa Mita tatu kwa mita mbili, sinki la maji, kutokutumia magogo kucharanga nyama na kutoruhusu wateja kugusa nyama wakati wa ununuzi.

Hata hivyo mwendesha mashtaka katika idara ya afya ya manispaa hiyo, Godfrey Meela alisema tayari manispaa hiyo imewaburuza mahakamani wafanyabiashara wanne ambao wameshindwa kutekeleza maagizo ya TFDA na manispaa hiyo kwa kutokidhi vigezo vya afya.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara katika soko kuu mjini Moshi wanaoza vyakula, Halina Abdala na Zuleha Kasimu walisema wamekosa wateja kutokana kukosa kitoweo hicho.
Michuzi Media Group

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa