Home » » LUSEKELO MCHAKATO WA KATIBA USITISHWE

LUSEKELO MCHAKATO WA KATIBA USITISHWE

Mchungaji Anthony Lusekelo  

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo, Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ amemtaka Rais Jakaya Kikwete kusitisha mchakato wa Katiba kwa lengo la kunusuru amani ya Taifa.
Lusekelo alisema siyo lazima Katiba Mpya ipatikane mikononi mwa Rais Kikwete kwa kuwa hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kubwa, hivyo inaweza kuendelezwa na Rais atakayefuatia mwaka 2015.
Akizungumza jana katika ibada ya Pasaka, Lusekelo alisema hali inayoendelea kwa sasa inajenga hofu na kuwachanganya Watanzania kutokana na hofu ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema Bunge la Katiba kwa sasa limekuwa mfano wa klabu ya pombe za kienyeji kutokana na vurugu alizodai kuchangiwa na wajumbe wa CCM.
“Hakuna majadiliano ya kujenga hoja na badala yake tunasikia matusi tu yanarushwa... uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kutoka nje ulikuwa ni sahihi. Hata mimi iwapo ningekuwa mjumbe, ningekuwa wa kwanza kutoka,” alisema Lusekelo na kuongeza:
“Kwa hiyo ni vyema mchakato ukasitishwa kwa hatua iliyofikia ili Taifa litulie na wananchi wajiandae kwa Uchaguzi Mkuu ujao.”
Iwapo mchakato huo hautasitishwa, alipendekeza busara zitumike kuunda jopo la watu kutoka Usalama wa Taifa na wataalamu wa masuala ya kiuchumi ili kujadili hoja tata ya muundo wa Serikali.
Alisema wachumi wanaweza kutafsiri hali ya uendeshaji wa uchumi wa nchi endapo serikali tatu zitapitishwa huku watu wa usalama wakitafsiri usalama wa nchi endapo muundo wa serikali mbili utakufa.
“Watu wa usalama wanaifahamu nchi hata kwa miaka 30 ijayo, wanajua usalama wa taifa hili utakuwaje, kwa hivyo wakikaa na wachumi wanaweza kuja na mapendekezo mapya tufanyeje,” alisema Lusekelo.
Lusekelo alisema: “Rais alikuwa na nia njema kabisa baada ya kuruhusu mchakato huu uanze, lakini kabla ya kuunda Tume inaonekana hakuwa amezungumza na chama chake juu ya mchakato wa Katiba, kwani kama angekuwa amewashirikisha yote haya yasingejitokeza.
“Tume aliyoiteua ilikuwa na watu makini sana kuanzia Mwenyekiti wake Jaji Joseph Warioba ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mkuu mstaafu Augustino Ramadhani na wenzake, ni wasomi wa sheria kwa hivyo walikaa na kuchambua mpaka wakaona muundo wa serikali tatu ndiyo unafaa.”
Alisema tatizo kubwa linalojitokeza ni pamoja na wajumbe wa CCM kulazimisha muundo wa serikali mbili ikiwa ni tofauti na uchambuzi uliofanywa na Tume hiyo.

Kakobe alia na Tanganyika
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe ametangaza kuungana na wanaodai Serikali ya Tanganyika na kuahidi kujenga ari na shauku ya kuhakikisha inarejeshwa.
Akizungumza wakati wa ibada ya Pasaka iliyofanyika kanisani hapo jana, Askofu Kakobe alisema anafanya hivyo si kwa ushabiki ila ni kutokana na mipango ya Mungu, ambayo iliwezesha kuwapo kwa Tanganyika huru. Huku akishangiliwa na waumini wa kanisa hilo, Askofu Kakobe alisema wanaoidai Tanganyika katika Bunge la Katiba wapo sahihi na yeye anaungana nao na kuwa wanaopinga wamekosa hofu ya Mungu.
“Serikali ilitumia mamilioni ya shilingi kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, lakini wanashindwa kutamka uhuru wa nchi gani!” alisema na kuongeza kuwa nchi imekosa utambulisho na hata Ziwa Tanganyika linawasuta kwa kuwa katika uumbaji kuna mipaka ya asili, ambayo inatambuliwa pia kitaalamu.
Kuzuia mabadiliko
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), mjini Moshi, Kilimanjaro, Glorious Shoo amewatahadharisha wajumbe wa Bunge la Katiba kutotumia wingi wao bungeni kuzuia mabadiliko ya Katiba.
Akizungumza katika ibada ya Jubilee ya miaka 75 ya kanisa hilo, Askofu Shoo alisema umefika wakati ambao Watanzania wanataka mabadiliko, hivyo wajumbe wa Bunge Maalumu wasitumie wingi wao kuzuia mabadiliko.
“Tusilazimishe kwa wingi wetu kuzuia mabadiliko kwa sababu ukweli tunaposema wingi wetu ni pale bungeni tu, lakini wingi wetu sisi tulioko nje tunasikia kelele nyingi  zinazolazimisha mabadiliko naiomba Serikali izingatie hilo,” alisema Askofu Shoo.
“Watu wanaosoma nyakati, wanajua ukifika wakati wa mabadiliko hakuna anayeweza kuzuia na ukijaribu kuyazuia mabadiliko hayo yanakuja kukubadilisha wewe,” alisema Askofu Shoo.
Akizungumza katika ibada hiyo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri aliwaomba viongozi wa madhehebu ya dini kufunga na kuliombea Bunge Maalumu la Katiba ili liweze kuifanya kazi ya kuchambua Rasimu ya Katiba kwa hekima itakayowapa Watanzania Katiba wanayoitaka.
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa