Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MKUU wa Mkoa (RC), wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, amewataka wapenzi
wa soka mkoani hapa kuweka siasa pembeni na badala yake waungane
kuisaidia Klabu Bingwa ya Mkoa, Panone FC inayojiandaa na mashindano ya
Ligi ya Mabingwa Mkoa (RCL), inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi
karibuni.
Gama ambaye ni mlezi wa klabu mkoani hapa, alitoa rai hiyo juzi
wakati akijibu kilio cha waandishi wa habari wa michezo Kilimanjaro,
ambao wengi walimtaka mkuu huyo kuhakikisha ofisi yake inasimamia
juhudi zote kuhakikisha klabu hiyo inapanda daraja.
Akizungumza katika tafrija fupi ya chakula pamoja na waandishi wa
habari, Gama alisema mwaka huu ofisi yake imejipanga kuhakikisha Panone
inafikia mafanikio yaliyofikiwa na Mbeya City na kuwataka wakurugenzi
na wakuu wa wilaya zote sita, kuwa tayari kwa kazi hiyo.
“Natambua ni kiasi gani mlivyo na uchungu na maendeleo ya soka mkoani
hapa, nitahakikisha timu hii inafanya vizuri, niwaombe viongozi
wenzangu bila kujali itikadi zetu, tuungane kwa hali na mali tuibebe
klabu hii,” alisema.
Gama ambaye amekuwa chachu ya kufufuka kwa hamasa ya michezo mkoani
hapa, alisema mwaka huu wamejifunza kutokana na makosa ya mwaka jana
wakati Machava wakiwa mabingwa, na kwamba safari hii kwa kushirikiana
na Chama cha Soka Mkoa (KRFA), atajitahidi kufanikisha azma hiyo.
“Mwaka jana tuliteleza kwa Machava, ni ukweli usiopingika kwamba
pamoja na tatizo la kiuongozi lililojitokeza katika klabu ile, siasa
zilichangia pakubwa kwa timu yetu kushindwa kupanda Daraja la Kwanza na
baadaye Ligi Kuu,” alisema Gama.
Wakizungumza katika hafla hiyo, waandishi Henry Lyimo, Dixon Busagaga
na Yusuph Mazimu, walimtaka Gama kuishauri Panone kuangalia upya,
kusuka uongozi wake na ikiwezekana kuunda kamati maalumu ambayo
itafanya kazi bega kwa bega na uongozi wa Panone kuhakikisha inafanya
vizuri.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment