Home » » WEZI NMB KUNYONGWA

WEZI NMB KUNYONGWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
  • Ni baada ya kupatikana na hatia ya kumuua askari polisi
Wezi NMB kunyongwaMAHAKAMA Kuu Kanda ya Moshi, imetoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa washitakiwa wawili raia wa Kenya, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya askari polisi PC Michael Milanzi.
Washitakiwa hao walimua askari huyo katika tukio la uporaji wa fedha katika Benki ya NMB, tawi la Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mbali na hukumu hiyo iliyosomwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kakusulo Sambo kwa zaidi ya saa nne, mshitakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Karisti Kanje (Mtanzania), amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kosa la kuhifadhi na kutorosha watuhumiwa wa mauaji ya askari polisi.
Akisoma hoja zilizotolewa mahakamani hapo na pande za utetezi na ile ya serikali, Jaji Sambo, alieleza kuwa ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na mashahidi 18 wa upande wa Jamhuri, mahakama iliridhika kuwa haukuacha shaka yoyote kwa washitakiwa wote watatu.
Alisema kutokana na ushahidi wa shahidi wa 1, 3 na 11, mahakama imeridhika kuwa washitakiwa wawili, Samwel Gitau Saitoti na mwenzake Michael Kimani, raia wa Kenya, walimuua kwa makusudi PC Milanzi kwa kumpiga risasi na kwamba inatoa adhabu kwa kila mmoja kunyongwa hadi kufa.
“Mahakama imeridhika kwa namna ambavyo mashahidi namba 1, 3, 11 walivyoelezea ushiriki wa washitakiwa katika tukio hilo. Mahakama imeridhika bila shaka yoyote kwamba washitakiwa hao walimuua kwa kukusudia askari wetu, ambaye serikali bado ilikuwa ikimhitaji,” alisema Jaji Sambo.
Alisema washitakiwa hao kwa pamoja wakiwa na lengo moja la kutekeleza ujambazi katika benki hiyo, waliamua kumuua PC Michael, kitendo ambacho kisheria adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa kwa mujibu wa kifungu 197 kanuni ya sheria namba 7.
Akieleza kwa kifupi maelezo ya shahidi namba 1, 3, na 11, ushahidi unaotajwa kuwa muhimu uliowatia hatiani washtakiwa hao, Jaji Sambo, alisema mashahidi wote walidai mahakamani hapo kuwa waliwaona wahusika wa mauaji kwa karibu na hakuna ubishi kuwa ndio walihusika na mauaji hayo.
“Shahidi namba tatu ambaye ni askari akiwa lindo na marehemu, aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa namba mbili (Kimani) alifika katika eneo la benki na kuomba kuonana na mmoja wa wafanyakazi waliokuwa bado ndani ya benki, ndipo marehemu akamuita mwenzake (shahidi namba 3) kwa mashauriano ambayo hata hivyo wote walikataa ombi hilo.
“Baada ya muda, nyuma ya kibanda ghafla akatokea mshitakiwa namba moja (Saitoti) akampiga kichwani PC Michael kwa kutumia kitako cha bunduki ndipo yakazuka mapambano, mshitakiwa namba mbili akipambana na shahidi, huku mshitakiwa namba moja akipambana na marehemu PC Michael,” alisema Jaji Sambo kueleza maelezo ya shahidi namba tatu.
Alisema muda wote wa mapambano shahidi alikuwa akitazamana ana kwa ana na washitakiwa, na kwamba baada ya kuzidiwa ndipo mshitakiwa namba mbili akasikika akimwambia mwenzake (mshitakiwa namba moja) afyatue risasi iliyompiga PC Michael na kuanguka chini.
Awali kabla ya kutoa hukumu hiyo, wakili wa upande wa utetezi, Faustine Materu, aliiomba mahakama ione kwamba miaka saba ambayo mshitakiwa namba tatu, Karisti Kanje aliyokaa gerezani, inatosha kuwa adhabu yake ombi ambalo hata hivyo lilipingwa na wakili wa upande wa serikali, Stella Majaliwa.
Tukio la uporaji na mauaji hayo lilitokea Julai 11 mwaka 2007 katika Benki ya NMB tawi la Mwanga, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa