Home » » JK ASHSURIWA KUTUPILIA MBALI MASHARTI YA UKAWA

JK ASHSURIWA KUTUPILIA MBALI MASHARTI YA UKAWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Rais Jakaya Kikwete
 
Mwavuli wa asasi za kiraia Mkoa wa Kilimanjaro umemshauri Rais Jakaya Kikwete kutoyakubali masharti yanayotolewa na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) nje ya Bunge  ya kutaka mwafaka naye Ikulu, kwa sababu mgogoro uliopo lengo lake si kupatikana kwa katiba mpya, bali ni ghiliba za kutaka kuking’oa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Viongozi wa asasi hizo 35 walitoa rai hiyo kwa Rais Kikwete juzi wakati walipokutana na mjumbe wa Bunge hilo, Elizabeth Minde, ambaye ni Wakili na Mwenyekiti wa CCM Wilaya Moshi.

Akizungumza katika mkutano huo, Taube Mabasi kutoka Wilaya ya Same, alisema wanaharakati nchini na baadhi ya viongozi wanaomshinikiza Rais Kikwete kumaliza mgogoro huo na Ukawa, hawataki kusema ukweli kuhusu ajenda ya kukwamisha mchakato wa upatikanaji wa katiba ili kutafuta huruma ya Watanzania katika uchaguzi mkuu ujao.

“Asasi za kiraia Kilimanjaro, tunamwomba Rais Kikwete asirudi nyuma, Watanzania wanataka katiba mpya. Ni kweli mabadiliko hayaepukiki, lakini tusivuruge basi huu mchakato ili Bunge livunjwe…Mabilioni ya kodi za Watanzania yanateketea bila huruma,” alisema Imaculate Mwozia kutoka Shirika la Kwieco.

Hata hivyo, Mchungaji Kusurie Massawe kutoka Shirika la Wodef Wilaya ya Siha, alisema athari zinazotokana na kuachwa kwa mgogoro uliopo kuendelea kuota mizizi baina ya Ukawa na upande unaounga mkono serikali mbili, ni kuingia katika uvunjifu wa amani.

“Tumwombe Mungu tupate katiba hiyo katika njia za maelewano. Lakini kama hali hii haitafikia mwisho, kutakuwa na balaa katika chaguzi zijazo. Kuna madai ya msingi, ambayo wenzetu wanatoa. Kwa hiyo, ni vizuri yakamalizwa kwa busara,” alisema Mchungaji Kusurie.

Mratibu wa Mwavuli wa Asasi hizo, Hillary Tesha, alisema miongoni mwa mambo, ambayo viongozi wa asasi hizo wamebaini ni pamoja na ubinafsi wa baadhi ya wanasiasa, ambao wametanguliza mbele maslahi ya chama, badala ya utaifa jambo, ambalo linatishia uhai wa demokrasia katika taifa.

Awali, Minde alisema baadhi ya wajumbe kutoka kundi la watu 201 hawafungamani na pande zinazogombea serikali tatu na mbili kwa kuwa wao wanataka katiba mpya itakayoliweka taifa katika amani kwa miaka 50 ijayo.

“Kutofautiana kimawazo kwa wanasiasa ni jambo la kawaida. Na nyie viongozi wa asasi za kiraia mtusaidie kuchoma sindano huko vijijini ili wananchi waelewe sisi tunapigania katiba ipatikane, lakini wanasiasa na baadhi ya wanaharakati hawapo pamoja na sisi,” alisema Minde.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa