Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mkoa wa
Kilimanjaro na Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo, amewaonya
baadhi ya Wanachama wa chama hicho wenye lengo la kukivuruga kwa misingi
ya kiitikadi.
Ndesamburo, alitoa onyo hilo wakati akifunga mkutano mkuu wa CHADEMA
Jimbo la Moshi Mjini uliyokwenda sanjari na uchaguzi wa kupata viongozi
wa jimbo hilo pamoja na mabaraza, juzi.
Alisema, kutokana na umoja uliyopo ndani ya CHADEMA Moshi Mjini,
baadhi ya watu kutoka nje ya chama wamekuwa wakijaribu kuwatumia
wanachama wa chama hicho kutaka kuwagawa katika misingi ya kiitikadi.
“Tumejaribiwa sana na watu kutaka kutugawa kwa udini, kutugawa kwa
ukabila, wanashangaa Jafary ni Mpare lakini ndiye Meya wetu, wengine
wanasema eti Meya Muislamu, sisi hatuchagui watu kwa sura zao wala
wanakotoka,” alisema Ndesamburo.
Aliutaka uongozi mpya uliochaguliwa juzi, kuanza kazi mara moja ya
kukiimarisha chama kuanzia ngazi ya mashina na kwamba, hadi kufikia
uchaguzi mkuu mwakani CHADEMA iweze kukamata dola.
“Ndugu zangu mmechaguliwa, sio kazi ya mchezo, msifurahie nafasi
mlizopata mkadhani ni lele mama, mmechaguliwa mkafanye kazi, sitegemei
kusikia mtu anasema sina nafasi, imani yangu kubwa kwa sasa tumepata
timu ya kuchapa kazi, tunataka Jimbo la Moshi liendelee kubaki CHADEMA,”
alisema Ndesamburo.
Naye Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Aman Golugwa, aliwataka
wazee wa Chama kwa hekima na busara zao, kuwashughulikia wanachama
watakaobainika kutaka kusababisha vurugu ndani ya chama.
“Uchaguzi umekuwa na heka heka nyingi, nafahamu kwa sasa tunaelekea
katika chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu, kwa wale wanaotaka
nafasi ya uongozi msituletee fujo, unataka nafasi ya uongozi ingia
kwenye mfumo wa chama, halafu tukupe nafasi ufahamike watu wakujue,”
alisema Golugwa.
Katika uchaguzi huo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Jafary
Michael, alifanikiwa kutetea nafasi yake ya Uenyekiti wa Jimbo la Moshi
Mjini baada ya kukosa mpinzani katika nafasi hiyo.
Katibu wa CHADEMA Jimbo la Moshi Mjini, alichaguliwa Stephen Buberwa,
Katibu Mwenezi Steven Ngasa huku mjumbe wa mkutano mkuu taifa akiibuka
Peter Msafiri.
Kwa upande wa wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji, walichaguliwa
Shaffi Ally, Cosmas Tesha, Paulo Minja na Aisha Rashid huku Baraza la
Vijana (Bavicha), wakichaguliwa Dominick Tarimo nafasi ya Uenyekiti,
Deogratius Kiwelu alishinda Ukatibu na Steven Urio Mhamasishaji Vijana.
Baraza la Wanawake walichaguliwa Mary Olomi (Mwenyekiti), Ovena Kowero (Katibu), Anna Mushi (Uenezi), na Nice Mushi (Mhazini).
Kwa upande wa Baraza la Wazee, walichaguliwa Ally Mwamba
(Mwenyekiti), Augustino Makelele (Mwenyekiti msaidizi), Ahmad Ndaile
(Katibu), na Mlavi Mrindoko (Mhazini)
Uchaguzi huo ni muendelezo wa chaguzi zinazoendelea nchi nzima, baada
ya kumaliza chaguzi za misingi, matawi na kata, ambako sasa hatua
inayoendelea ni ya ngazi ya majimbo/wilaya kuelekea Mikoa na Kanda,
kabla ya uchaguzi wa viongozi wa kitaifa unaotarajiwa kufanyika baadaye
mwaka huu.
Chanzo:Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment