Home » » DKT. MALASUSA AVUNJA UKIMYA

DKT. MALASUSA AVUNJA UKIMYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

WAKATI Taifa likiwa katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dkt.

Alex Malasusa, amesema Kanisa hilo halipo tayari kuvumilia mifumo inayominya haki za wananchi na uhuru wa kuishi kwa amani.

Dkt. Malasusa aliyasema hayo jana wakati akiwasilisha neno kuu katika Mkutano Mkuu wa 33 wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa hilo unaoendelea katika Chuo Kikuu cha Stephano Moshi (SMMUCO), kilichoko mkoani Kilimanjaro.

Alisema jamii inayoongozwa na mifumo ya uonevu, hupoteza uzalendo ambapo nchi yenye mifumo ya namna hiyo, kauli ambazo hutumika ni zile za ‘mwenye nguvu mpishe apite’.

“Wenye nguvu huishi bila huruma wala chembe ya ubinadamu kwa wenzao wanyonge...Kanisa haliwezi kuwa kimya kwa mifumo ya aina hii, hata sasa kuna taarifa mbalimbali zinazodai mwenye fedha au uwezo wa aina yoyote, akikamatwa hakai ndani huachiwa mapema kutokana na uwezo wake kifedha ukilinganisha na wanyonge,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika mifumo ya namna hiyo kwenye maisha, mwenye nguvu au uwezo akikosea badala ya kuchukuliwa hatua zinazostahili, yeye ndiye anayeamua hatima ya kosa alilolifanya ambapo mifumo ya namna hiyo, husababisha nchi kukosa mwelekeo na watawala kukosa misimamo thabiti.

Alitoa wito kwa waumini wa Kanisa hilo na Watanzania wote, kutokata tamaa kutokana na hali ngumu ya maisha akiwataka wazidi kuliombea Taifa liweze kuendelea na hali ya utulivu uliopo.

“Kama ilivyokuwa enzi za Yohana wa Patimo, jamii yetu kwa sasa inapitia Patimo nyingi yenye maisha magumu, maadili yameporomoka, utamaduni wetu umeanza kuporomoka na heshima imetoweka, kilichobaki ni kumwomba Mungu na kumtegemea ili turudie hali ya uwepo wa maadili mema”, alisema.

Akizungumzia maombezi na huduma zingine za Kanisa, Askofu Dkt. Malasusa alisema kuna baadhi ya watu wamegeuza suala la maombi kuwa duka la kujipatia mapato.

“Wakati wa mateso na shida mbalimbali zinazomkabili mwanadamu,hutokea watu wanaojidai Manabii na Mitume, uzalendo hutoweka na jamii kuongozwa kwa vitisho,” alisema.

Kuhusu utandawazi, alisema pamoja na nia njema ya kukua kwa teknolojia, baadhi ya watu wameamua kuitumia vibaya fursa hiyo kutokana na kutoandaliwa vizuri katika kupokea teknolojia husika.

“Kuna watu ambao huingia Kanisani na simu na kuanza kuitumia katika kufuatilia Ibada kwa sababu ya kuhifadhi maandiko ya Biblia

Takatifu kwenye simu zao... pamoja na mawazo yao mazuri huwa inaondoa maana halisi ya ushiriki katika Ibada, si dhambi kufanya hivyo ila si mwenendo mzuri,” alisema.

Mkutano huo unaotarajiwa kumalizika kesho umekuwa ukiongozwa na neno kuu linalosema; “Tazama nayafanya yote kuwa mapya”.

 Chanzo;Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa