Home » » JWTZ YAZINDUA ZOEZI KUBWA LA KIVITA MONDULI

JWTZ YAZINDUA ZOEZI KUBWA LA KIVITA MONDULI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Kikosi cha Ardhini cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kikiwa kwenye mazoezi maalumu katika kambi ya Msangani, iliyoko Kibaha, mkoani Pwani jana. Kikosi hicho na vikosi vingine vya jeshi hilo vinafanya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya JWTZ yatakayofanyika Monduli, Arusha Sepemba 5, mwaka huu. PICHA: NDENINSIA LISLEY
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limezindua zoezi kubwa la kivita linayoishirikisha Divisheni moja ya kijeshi.
Zoezi hilo linalofanyika katika eneo la Monduli, mkoani Arusha, ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa JWTZ Septemba mosi, 1964.

Divisheni hiyo inaundwa na makamanda na wapiganaji kutoka Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu, Kamandi ya Jeshi la Anga, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Akiba.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk. Hussein Mwinyi, aliwataka washiriki kutumia weledi wao kwa umakini ili malengo ya zoezi hilo ya medani yafikiwe.

“Hili ni la muhimu katika kulifanya jeshi letu liwe katika hali ya utimamu na uwezo mzuri wa kimapigano,” alisema.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, alisema madhumuni ya mazoezi hayo, pamoja na mambo mengine, ni kupima na kujenga uwezo wa utendaji wa pamoja wa JWTZ katika kukabiliana na adui kivita, kwenye nchi kavu na anga.

“Zoezi hili linalenga kuinua uwezo wa kupanga na kutekeleza jukumu la kivita kwa makamanda na askari wetu katika zoezi la pamoja, kujiweka tayari kukabiliana na adui halisi, na kupima uwezo wa uhamasishaji na usambaratishaji na mengineo,” alisema

Naye Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu na aliye Kamandi Mkuu wa zoezi hilo, Meja Jenerali Salum Kijuu, alisema zoezi hilo linahusisha silaha mpya na zana mbalimbali za kimapigano kama ndege vita, vifaru na magari ya delaya.

“Lakini pia wahandisi na vikundi vya lojistiki na litakamilika kwa kufanya shambulio la kukusudia,” alisema. Kwa mujibu wa Meja Jenarali Kijuu, zoezi hilo lililoanza jana linatarajiwa kumalizika Septemba 5, mwaka huu.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa