CHAMA
cha ushirika wa masoko na mazao ya kilimo cha Kirua Vunjo Kaskazini,
(Kirua Vunjo North Amcos), cha Moshi Vjijini, mkoani Kilimanjaro,
kinatarajia kupata mapato ya ziada ya sh. milioni 4.8, katika msimu wa
2014/2015.
Hayo yameelezwa na
mwenyekiti wa chama hicho Bw. John Chaki, wakati akizungumza na
wanahabari, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, hivi karibuni.
"Ziada hii itatokana na
mapato ya jumla ya zaidi ya shilingi milioni 15 tunayotarajia kuyapata
katika kipindi hiki," alisema na kuongeza kuwa wanachama wa chama hicho
tayari wameridhia kujiunga na mfumo mpya wa kukusanya kahawa kwa
kujitegemea.
Aliongeza, "Ili
kufanikisha zoezi la kujitegemea katika mfumo huu mpya, wanachama
wamepitisha ukomo wa madeni wa shilingi milioni 120 kutoka benki ya
ushirika mkoani Kilimanjaro (KCBL), kwa ajili ya kukusanyia kahawa
katika msimu huu mpya."
Awali meneja masoko wa
KCBL Bw. Asanterabi Msigomba, alisema benki hiyo tayari imeshaandaa
mikakati inayolenga kuviwezesha vyama vya ushirika wa masoko na mazao ya
kilimo vilivyojiunga na mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani.
Aidha alitoa wito kwa
vyama vya ushirika masoko na mazao ya kilimo kujenga tabia ya kuwalipa
wakulima fedha zao punde wanapowasilisha mazao yao ili waweze
kujiendeleza ikiwamo kulipa fedha walizokopa kwa ajili ya kuimarisha
kilimo na kuongeza uzalishaji wa mazao.
"Kosa kubwa ambalo
linaweza kudhoofisha juhudi za kilimo ni kutokumlipa mkulima kwa wakati
na wakulima kuuza mazao nje ya mfumo wa chama, mambo haya hudhoofisha
mfumo mzima unaolenga kuongeza tija katika kilimo," alionya.
Bw. Msigomba pia
alielezea umuhimu wa mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ulioasisiwa na
benki hiyo ya kwanza ya ushirika hapa nchini ambapo alisema tayari
taasisi hiyo ishatoa mafunzo kwa vyama vya ushirika wa masoko na mazao
ya kilimo (Amcos), kuhusu mfumo huo.
0 comments:
Post a Comment