Home » » MADIWANI WAKOSA IMANI NA KITUO CHA POLISI

MADIWANI WAKOSA IMANI NA KITUO CHA POLISI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, limedai kukosa imani na Kituo Kidogo cha Polisi Ngulu kilichopo Kata ya Kwakoa, wakidai askari wake si waadilifu.

Baadhi ya askari wa kituo hicho kwa kushirikiana na mgambo, wanadaiwa kukusanya fedha kutoka kwa wananchi bila kuwapa stakabadhi pamoja na kuwanyanyasa.

Akizungumza katika kikao cha baraza hilo, Diwani wa Kata ya Kwakoa, Tarafa ya Jipendea, Rogers Msangi, aliliomba Jeshi la Polisi mkoani humo kuwachunguza askari hao kwani wanachangia kulifedhehesha jeshi hilo na kuondoa imani kwa wananchi.

Alisema kero dhidi ya askari na mgambo kituoni hapo, aliziwasilisha kwa Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) lakini hakuna hatua alizochukua.

"Sielewi kiburi walichonacho askari na mgambo katika kituo hiki wanapata wapi, nimepeleka malalamiko mara nyingi kwa OCD lakini hakuna hatua zinazochukuliwa," alisema.

Katika hatua nyingine, Msangi aliiomba halmashauri hiyo kuharakisha mchakato wa kupata gari la wagonjwa katika tarafa hiyo akisema amekuwa akitumia gari lake binafsi kubebea wagonjwa.

Aliongeza kuwa, kukosekana kwa gari la wagonjwa katika tarafa hiyo yenye kata za Kivisini, Jipe na Butu, kunasababisha adha kwa wagonjwa na kuhatarisha maisha yao hasa wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.

Naye Diwani wa Kata ya Shighatini, Enea Mrutu, alisema vitendo vinavyofanywa na polisi na mgambo katika kituo cha Ngulu havipaswi kufumbiwa macho kwani huenda vikahatarisha amani.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Theresia Msuya alisema halmashauri inatambua mahitaji ya gari la wagonjwa na kwamba kero hiyo itapatiwa ufumbuzi baada ya Wilaya kupokea gari la wagonjwa kutoka serikalini.

Akijibu suala la Kituo cha Polisi Ngulu, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, William Msapali, alisema kero hiyo imefikishwa katika Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya kwa ajili ya utatuzi

 Chanzo:Majira

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa