Home » » MBATIA AISHANGAA SERIKALI KUKOSA KIPIMO CHA EBOLA

MBATIA AISHANGAA SERIKALI KUKOSA KIPIMO CHA EBOLA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

Balozi  wa Majanga Afrika, James Mbatia, amesema Serikali‘inajifedhehesha kwa kushindwa kuisaidia Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na kutokuwa mtambo wake wa  kuchunguza sampuli za damu za wagonjwa wakiwamo wanaohisiwa kuwa na virusi vya Ebola kutegemea vipimo vya Kenya.

Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alisema kwa Wizara ya Afya kukiri kwamba vipimo hivyo huchukuliwa na kupelekwa Nairobi kwa ajili ya uchunguzi zaidi ni fedheha kwa taifa ambalo linajinasibu limepeleka Afrika ya Magharibi timu ya madaktari bingwa watano kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Akiwa Kata ya Mamba Kusini, Wilaya ya Moshi, Mbatia aliwaambia wakazi wa eneo hilo kwamba Serikali bado haijaonyesha nia ya dhati ya kujikinga na maambukizi ya Ebola na wala haijutii gharama kubwa inazotumia kupeleka nje ya nchi sampuli hizo kwa ajili ya vipimo.

“Serikali yetu haina lugha moja kuhusu ugonjwa huu na bado ingali inajifedhehesha kutokana na Muhimbili kukosa mashine ya kuchunguza sampuli za damu zenye virusi vya ugonjwa wa Ebola. Je, nani tumbebeshe mzigo huu?” alihoji.

Pamoja na kuikosoa Serikali, Mbatia alimkabidhi Makamu Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Sh. milioni 10 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa nyumba za walimu wa Shule ya Sekondari ya Stephano Moshi.

Wiki iliyopita, mfanyabiashara mmoja (jina limehifadhiwa) ambaye alitokea nchini Senegal, alizua taharuki kwa wakazi wa mji wa Moshi baada ya kuugua homa kali iliyohusishwa na Ebola na kulazimika kuwekwa karantini katika Zahanati ya Shirimatunda iliyopo mjini hapa.

Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii jana ilitoa taarifa ikisema kwamba majibu ya vipimo vya mgonjwa aliyewekwa karantini, yamerejea toka Kenya kuwahakikishia wananchi kwamba mfanyabiashara huyo hana Ebola.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa