Home » » KERO YA MAJI MOSHI MWISHO DESEMBA

KERO YA MAJI MOSHI MWISHO DESEMBA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi Mjini (MUWSA), inatarajiwa kukamilisha utekelezaji wa miradi mitatu ya maji ambayo itaondoa kero ya muda mrefu kwa wananchi ifikapo Desemba mwaka huu.
Hayo yamebainishwa kwenye taarifa ya hali ya huduma ya maji safi iliyotolewa juzi na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo, Cyprian Luhemeja, katika mkutano maalum na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa mamlaka hiyo mjini hapa.
Miradi hiyo inahusisha visima viwili vya CCP na ‘Kili Tank’ pamoja na chanzo cha maji kilichopo Mto Karanga, ambacho maji yake yatazinufaisha Kata za Pasua, Boma Mbuzi, Matindigani, Mabogini na maeneo ya katikati ya mji, ambako wananchi wapatao 20,000 watanufaika.
Alisema mradi huo wa maji kutoka chemchem ya chanzo cha maji Mto Karanga, unategemewa kuongeza mita za ujazo 2,592 kwa siku katika mfumo wa kusambazia maji pindi mradi utakapokamilika.
Kwa mujibu wa Luhemeja, uzalishaji wa maji katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita ni wastani wa mita za ujazo 34,944 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya mita za ujazo 45,082.
Mamlaka hiyo pia imefanya ukarabati wa kilometa 11.8 za mabomba katika mkakati wa kuhakikisha maji yanayoongezwa kwenye mfumo wa kusambazia hayapotei kwa kupitia kwenye mabomba chakavu na hivyo kuwafikia wateja wengi zaidi.
Mkurugenzi huyo, alisema matarajio ya mamlaka yake kipindi cha Oktoba 2014 na Juni 2015, ni kuanza ujenzi wa chemchem ya maji ya Ndesuo iliyopo Kibosho Wilaya ya Moshi Vijijini katika mpango wake wa kuboresha zaidi huduma ya maji safi.
Mpango mwingine wa mamlaka hiyo ni kumalizia uchimbaji wa visima viwili vya maji vilivyopo Kata ya Longuo, ambavyo MUWSA ilikabidhiwa na Manispaa ya Moshi ikiwamo uwekaji wa umeme, pampu, ‘mota’ na mabomba.
Chini ya mpango huo, MUWSA imelenga kufanyia ukarabati mtandao wa majisafi kwa  kilometa 14.9 pamoja na upanuzi wa mtandao kwa kilometa 40.65 katika sehemu mbalimbali za mji ambazo bado hazijafikiwa na mtandao.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa