Home » » MAHAKAMA YAMBANA MKURUGENZI MOSHI

MAHAKAMA YAMBANA MKURUGENZI MOSHI

Mahakama ya Hakimu Mkazi-Moshi mkoani Kilimanjaro, imemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya manispaa hiyo, Shaaban Ntarambe, kufika mbele ya mahakama hiyo kujieleza ni kwa nini asipewe adhabu kali kwa kudharau amri halali ya mahakama ya kumuita shaurini.

Ntarambe aliyetakiwa kufika mahakamani hapo jana, aliandikiwa hati ya wito iliyosainiwa na kugongwa muhuri wa Hakimu Mkazi Mfawidhi-Moshi, Januari 8, mwaka huu, ikimtaka yeye binafsi au wakili wake, kufika mbele ya mahakama hiyo Januari 13, mwaka huu saa 3:00 asubuhi kwa kesi inayomkabili.

Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Julieth Mawole, aliwataka wanasheria wawili wa Halmashauri ya manispaa hiyo, Sylivia Shayo na Apolinary Msaki, wanaomwakilisha Mkurugenzi huyo, kuieleza mahakama sababu za Ntarambe kushindwa kutii amri halali ya mahakama.

Mwanasheria wa Manispaa, Shayo, aliieleza mahakama hiyo kwamba Ntarambe alishindwa kufika mahakamani hapo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake.

“Lengo la kumuita mahakamani Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi ni moja tu; ni kumuuliza ni kwa nini asipewe adhabu kali kwa kushindwa kutii amri ya mahakama lakini kwa sababu wanasheria waliomwakilisha wamesema ameshindwa kufika mahakamani kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake; naahirisha shauri hili (bila ya kutaja tarehe) na nitawataarifu wadai wa shauri hili siku ya kufika mahakamani,” alisema Hakimu Mawole.

Mkurugenzi huyo anakabiliwa na kesi ya kukamata isivyo halali malori matatu yaliyokuwa yamebeba mananasi, Desemba 18, mwaka jana akidaiwa fidia ya Sh. milioni 54.

Wadai katika kesi hiyo ni Malaki Mmari, Abdul Ramadhan, Shaaban Juma na Goodluck William.

CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa