Home » » MADIWANI MOSHI SASA WAMNING’INIZA MKURUGENZI

MADIWANI MOSHI SASA WAMNING’INIZA MKURUGENZI

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
 Tuhuma za rushwa na uporaji wa mali za Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, zimesababisha vurugu zilizopelekea kikao cha Baraza la Madiwani kumkataa Mkurugenzi, Shaaban Ntarambe, huku likipitisha azimio la kumburuza mahakamani kwa ubadhirifu.
 
Meya wa Manispaa hiyo, Jaffary Michael, akizungumza mara baada ya kuvunjika kwa Kikao cha Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Manispaa hiyo kwa mwaka 2015/2016, alisema madiwani hao wamepanga kumwandikia barua Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (pichani), wakimtaarifu kuhusu hatua watakazochukua dhidi ya Mkurugenzi huyo, ikiwamo kufungua mashtaka mahakamani.
 
“Tumetenga zaidi ya Sh. milioni 124 kwa ajili ya kufanya usajili wa viwanja vyetu, lakini fedha hiyo hiyo imeanza kutuletea balaa,
Madiwani wangu wamejiridhisha, nami ni shahidi,” alisema.
 
Alisema Mkurugenzi amehusika baada ya kuondoa kwa siri, zuio la Baraza kwa Msajili wa Hati na kutengeneza hati kwa ajili ya kuwapatia matajiri wachache waliojificha nyuma ya kikundi, kinachojiita Mawenzi Sports Club, akishirikiana na watendaji …viwanja vyote vya umma vilivyobaki havina hati haviko salama tena,” alisema Meya.
 
Kabla ya kuvunjika kwa kikao hicho, ambacho kilihudhuriwa pia na Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi (Das), Remida Ibrahim, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya; Diwani wa Kata ya Rau (Chadema), Peter Kimaro, baada ya sala alimshambulia Ntarambe, akidai amehusika katika uporaji wa uwanja wa Mawenzi wenye hati namba 10660 (056035/12).
 
Baada ya hoja hiyo, madiwani 24 kati ya 29 wanaounda Baraza hilo, walitoka nje wakitaka Mkurugenzi huyo awajibike kwa kujiuzulu wadhifa wake au aondoke Moshi kabla ya kumburuza mahakamani.
 
Mgogoro huo ulilipuka zaidi baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji, Ardhi na Mazingira, Rey Mboya, kudai eneo hilo limeporwa kutokana na nguvu ya watendaji kuamua kutengeneza hati nyingine kinyemela.
 
Wakati vurugu hizo zikitokea, madiwani wanne wa CCM, Apaikunda Naburi (Mawenzi),  Priscus Tarimo (Kilimanjaro), Miriam Kaaya (Viti maalum) na Michael Mwita (Kaloleni), walijibizana kwa maneno makali na Meya kwa madai ameshindwa kutenda haki kwa kumruhusu Tarimo kuuliza swali kabla ya kuanza kwa kikao.
 
Mbunge wa Moshi Mjini (Chadema), Philemon Ndesamburo, alisema licha ya Halmashauri hiyo kuongozwa na Chadema, hawawezi kuungana na kukubali watendaji wachache na baadhi ya wanasiasa kuiba mali za umma.
 
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Halmashauri hiyo, Mkurugenzi wa Mipango Miji na Ramani wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mwaka 2001 aliidhinisha eneo hilo ni mali ya umma baada ya kupigwa kwa picha za anga kati ya mwaka 1998 na 1999.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa