Home » » WANA CCM WAMJIA JUU NAPE

WANA CCM WAMJIA JUU NAPE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Nape Nnauye
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi, Nape Nnauye
MRATIBU wa marafiki wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa walioko Kanda ya Kaskazini, Noel Nnko, amesema kauli ya Katibu wa Halmshauri Kuu,Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, dhidi ya makundi yanayokwenda nyumbani kwa kiongozi huyo kumshawishi agombee urais ni ya udhalilishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Nnko alisema kitendo cha Nape kusema wanaokwenda kwa Lowassa wanapewa fedha ni cha udhalilishaji kwa kuwa hakuna ushahidi wowote juu ya hilo.
“Viongozi wanatakiwa kufanya utafiti kabla ya kuzungumza kwa sababu matamko mengine yanadhalilisha na kujenga chuki katika jamii. “Pamoja na hayo, kama Nape aliona Lowassa anakosea kuwaruhusu wananchi wanaofika nyumbani kwake, angefuata utaratibu kwa kutumia vikao vya chama katika kujadili jambo hilo.
“Lakini ikumbukwe kwamba Mwenyekiti wetu Rais Jakaya Kikwete aliposema tumshawishi kiongozi tunayemwona anafaa katika urais, hakusema tutumie utaratibu gani.
“Hakusema tutumie barua, tutumie njia za mitandao ya kijamii au njia nyingine, alisema tuwashawishi watu na sisi tumeona tukamshawishi ana kwa ana,” alisema Nnko.
Naye Mwenyekiti mstaafu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mkoa wa Kilimanjaro, Godliving Mosha, alisema wanachofanya vijana pamoja na wananchi wengine nchini ni mapenzi yao na hakuna ushawishi wa Lowassa katika hayo.
Alisema ni vema CCM wakaheshimu uamuzi unaofanywa na wananchi ili kuondoa tabia ya wananchi kurushiana maneno bila sababu za msingi. Kauli za viongozi hao zimekuja siku chache baada ya Nape kupinga utaratibu wa watu kwenda nyumbani kwa Lowassa, Dodoma na Arusha wakisema wanakwenda kumshawishi agombee urais mwaka huu.
Wakati huo huo, Nape jana alimpongeza Lowassa kwa kukubali kusitisha makundi ya Watanzania wanaokwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee urais.

Akizungumzia uamuzi huo wilayani Same mkoani Kilimanjaro jana, Nape alisema Lowassa amefanya jambo zuri kwa kukubali kutii maagizo ya chama na kanuni zinazokiongoza.
“Nampongeza Lowassa kwa kukubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama ambayo ndiyo inatakiwa kufuatwa na kila mmoja ndani ya chama.
“Alichokuwa anafanya Lowassa ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa mujibu wa chama chetu ni makosa maana anakiuka taratibu na kanuni za chama. Hatuwezi kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa. Kwahiyo nampongeza kwa kutii agizo la chama,” alisema Nape.
Chanzo:Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa