Home » » Mrema awataja Kinana, Mbatia TLP.

Mrema awataja Kinana, Mbatia TLP.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustino Mrema.
Chama cha Tanzania Labour (TLP), kimefanya mkutano mkuu wa uchaguzi huku mwenyekiti wake wa Taifa, Augustino Mrema, akitumia muda mrefu kumshutumu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, kwamba wanakihujumu chama hicho ili kianguke.
 
Alisema hayo jana wakati wa mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa lengo la kumchagua mwenyekiti wa Taifa na kumuidhinisha mgombea urais atakayepeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
 
Mrema alisema Kinana alipofanya ziara katika Jimbo la Vunjo alisema uongo kwa kuwaeleza wananchi kwamba fedha za mfuko wa jimbo zilizopelekwa na serikali katika jimbo hilo kwa miaka minne ni Sh. milioni 400 wakati ni Sh. milioni 150 tu.
 
“CCM wameamua kuishi kwa uongo, nani atawaheshimu, nani atamuheshimu Kinana, mbona anamdhalilisha Rais Kikwete, Kinana hafai mbona tembo wanauawa na meno ya tembo yanaibwa lakini hasemi haya anakaa kimya,” alisema.
 
Alisema Kinana anashangaza Watanzania kwani katika ziara zake hazungumzii viongozi waliokula fedha za akaunti ya Tegeta Escrow badala yake anaiandama TLP na Mrema na kwamba hata akifanya hujuma hizo kamwe hataweza kuangushwa katika jimbo la Vunjo.
 
“Kinana anatukana mawaziri Rais amekaa kimya hamkemei, Kinana anatumia fedha nyingi kunichafua na sijui kama ni fedha halali, Rais usinyamaze watu wa Vunjo hawatakubali kuona hujuma zinazofanywa na Kinana dhidi ya TLP,” alisema.
 
Mrema alisema kutokana na hali hiyo amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kumlalamikia Kinana kwa kauli zake kwamba amejilimbikizia madaraka na kumuomba Rais achukue hatua.
 
Kuhusu Mbatia, alidai kuwa amekuwa akiendesha kampeni chafu ya kuichafua TLP ambazo zimepewa jina la ‘delete (futa) TLP’ katika jimbo la Vunjo kiasi cha kusababisha baadhi ya viongozi wa TLP kuhamia NCCR-Mageuzi.
 
“Kuna madiwani wa TLP ambao waliasi hadharani na wakawa wanampigia debe Mbatia na waliingia katika kampeni hiyo na walikuwa wakidai uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni uamuzi wa Mungu,” alisema.
 
Alisema watu ambao wamekuwa wakimuombea mabaya afe ili wagombee jimbo la Vunjo wahesabu kuwa wameumia kwani hivi sasa yupo ‘fiti’ na kuwahakikisha wajumbe wa mkutano huo kwamba atagombea jimbo hilo na kuchaguliwa kwa mara nyingine tena.
NIPASHE ilimtafuta Kinana ajibu tuhuma hizo, lakini simu yake ya mkononi mara kadhaa ilikuwa ikiita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) hakujibu.
 
Dakika 10 baada ya kutumiwa sms alipotafutwa simu yake ilizimwa.
 
Mbatia alipopigiwa simu yake ilikuwa inaita bila kupokelewa na alipotumiwa sms alijibu kuwa yupo kwenye mkutano.
Mrema akizungumzia hali ya usalama nchini alisema Taifa linakabiliwa ombwe la uongozi na kwamba hali ya usalama siyo nzuri kwani kuna matatizo mengi ambayo hayajapatiwa ufumbuzi wa kudumu ikiwamo mauaji ya albino, uvamizi wa vituo polisi unaosababisha mauaji ya polisi.
 
“Hali ya kisiasa katika nchi si nzuri, nchi inaelekea kubaya, kuna matatizo mengi kama vile ugaidi, udini, mauaji ya albino, uvamizi wa vituo vya polisi, mauaji ya polisi na kuporwa bunduki. Sioni kiongozi anayejitokeza kukabiliana na matatizo hayo,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa