Home » » MAHAKAMA YAPOKEA BARUA INAYOBISHANIWA.

MAHAKAMA YAPOKEA BARUA INAYOBISHANIWA.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Erasto Msuya
Mahakama  Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi, imepokea barua ya makabidhiano ya vielelezo vya kesi ya mauaji ya mfanyabiashara, bilionea wa madini ya Tanzanite, Erasto Msuya (43), (pichani, iliyotolewa na shahidi wa tisa, Inspekta Samuel Maimu (45) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kilimanjaro (RCO).
 
Jaji Salma Maghimbi alipokea kielelezo hicho jana, hivyo kumaliza ‘utata’ wa mapingamizi yaliyotolewa na upande wa utetezi, unaodai barua hiyo imepikwa na kutiwa saini na mtu mwenye vyeo viwili vya Jeshi la Polisi.
 
Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Hudson Ndusyepo, walidai  kutokana na mazingira ya kesi hiyo, polisi hawakuzingatia kanuni za makabidhiano siku ya tukio hilo. Kwa sababu hiyo, walidai upande wa mashtaka wametengeneza barua baada ya kuona mwanya wa kuibuka kwa mapingamizi.
 
Msuya aliuawa kwa kupigwa risasi Agosti 7, 2013, saa 6:30 mchana katika eneo la Mijohoroni, kando kando ya Barabara Kuu ya Arusha-Moshi, karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).
 
Kesi hiyo namba 12, ya mwaka 2014; inawakabili washtakiwa Sharif Athuman (31), ambaye ni mfanyabiashara wa madini na mchimbaji mdogo, mkazi wa Kimandolu mkoani Arusha, Shaibu Saidi maarufu kama “Mredii” (38) mkazi wa Songambele, Simanjiro mkoani Manyara na Mussa Mangu (30), Shangarai kwa Mrefu.
 
Wengine ni Jalila Said (28), mkazi wa Babati, Sadiki Jabir a.k.a “Msudani” (32), mkazi wa Dar es Salaam na Lang’ata, Wilaya ya Hai, Karim Kihundwa (33), mkazi wa Lawate, Wilaya ya Siha na Alli Musa maarufu “Mjeshi”, mkazi wa Babati, mkoani Manyara.
 
Kabla ya kuibuka kwa mabishano hayo ya kisheria kati ya utetezi na upande wa mashtaka, Wakili Mwandamizi wa Serikali Abdalah Chavula, alianza kwa kwa kumwuliza maswali Inspekta Samuel kama ifuatavyo.
 
Wakili: Hebu tukumbushe tarehe 7/8/2013 ulifanya yepi?
 
Shahidi: Siku hiyo nikiwa kwenye tukio, nilikusanya vielelezo, kuchora ramani na kuondoa vielelezo katika eneo la tukio.
 
Wakili: Ni vielelezo vipi ulikusanya katika eneo la tukio?
 
Shahidi: Vielelezo nilivyovikusanya siku hiyo vilikuwa gari, SMG (bunduki), maganda ya risasi, bastola ya marehemu, magazini mbili, simu mbili za marehemu na tablet (komyuta ndogo) moja ya marehemu.
 
Wakili: Baada ya kuwa umevikusanya vielelezo hivyo, ulifanya nini?
 
Shahidi: Gari nililipeleka kituo cha Polisi Bomang’ombe lakini vielelezo vingine vyote vilikuwa chini ya uangalizi wangu.
 
Wakili: Ni gari gani ambalo mlilitumia kuhifadhi vielelezo hivyo?
 
Shahidi: Toyota Land Cruiser.
 
Wakili: Kulikuwa na bahasha ngapi ambazo mlitumia kuhifadhi vielelezo hivyo?
 
Shahidi: Vielelezo tulivyovihifadhi ilikuwa ni bunduki, bastola, magazini na maganda ya risasi tuliweka katika bahasha yake kila kimoja.
Wakili: Hebu tuambie mliokota maganda mangapi ya risasi?
 
Shahidi: Tuliokota maganda 22 ya risasi.
 
Wakili: Kwenye hizo magazini kulikuwa na risasi ngapi?
 
Shahidi: Magazini ndogo ilikuwa na risasi 7, na magazini kubwa ilikuwa na risasi 23.
 
Wakili: Unaweza ukaieleza mahakama ni namba gani ulii-label (kuipa alama) hiyo kesi?
 
Shahidi: Nilii-lable (kuipa alama) kwa namba Bomang’ombe/KR/ 2786/ 2013.
 
Wakili: Uliendelea kukaa na vielelezo hivyo hadi lini?
 
Shahidi: Nilikaa na vielelezo hivyo hadi tarehe 8/8/2013 ambayo ilikuwa siku ya pili ya tukio hilo.
 
Wakili: Baada ya hapo nini kilitokea?
 
Shahidi: Nilitoa simu mbili na kumkabidhi Detective Constebo William kwa ajili ya kwenda kufanya uchunguzi (Cyber Crime) na baadaye vielelezo vingine nilivikabidhi kwa RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa).
 
Wakili: Siku hiyo ya tarehe 8/8/2013 ulimkabidhi Afande William simu ngapi?
 
Shahidi: Nilimkabidhi simu mbili na tablet, lakini hiyo tablet alinirudishia akisema hana kazi nayo.
 
Wakili: Ni simu gani mlikabidhiana na Afande William?
 
Shahidi: Zilikuwa Iphone 5 na Sumsung.
 
Wakili Chavula: Kama ni kujikumbusha ungependa ujikumbushe kwenye nini?
 
Shahidi: Nilikuwa na dayari na niliandika pia katika karatasi nyingine, kama mahakama ikiniruhusu naweza kuangalia katika hiyo karatasi.
 
Wakili: Shahidi hiyo dayari iko wapi?
 
Shahidi: Wakati nahama Moshi mjini kwenda Kituo cha Polisi Himo, nili-misplace (sikujua niliiweka wapi), lakini baadaye niliiona ikiwa imeharibika na maandishi yake yanasomeka kwa mbali. Lakini wakati huo nilikuwa nimeandika notes katika karatasi nyingine.
 
Wakili: Kwa hiyo kwa sasa, iko wapi?
 
Shahidi; Iko nyumbani Himo lakini ni ya kutafuta.
 
Wakili: Shahidi, makabidhaiano yenu mliyafanya katika mfumo upi?
 
Shahidi: Tulitumia barua kama hati maalum.
 
Wakili: Je, ungependa tuitoe barua hiyo mahakamani kama kielelezo?
 
Shahidi: Ndiyo, ningependa itolewe kama kielelezo.
 
Baada ya mwongozo huo wa maswali kutoka kwa Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula, jopo la mawakili wa utetezi lilisimama na kuanza kutoa sababu za kupinga kupokewa kwa barua hiyo ya makabidhiano kama kielelezo cha ushahidi kama ifuatavyo.
 
Moja, Wakili Ndusyepo alidai kuwa wakati mwandishi wa barua hiyo ambaye ni RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kilimanjaro), anaitia saini kwa ajili ya makabidhiano, alikuwa na cheo cha SSP (Mrakibu Mwandamizi wa Polisi), lakini kwenye barua iliyowasilishwa mbele ya mahakama pia inaonyesha alifanya hivyo  akiwa na cheo cha ACP (Kamishna Msaidizi wa Polisi), ambapo kwa wakati huo hakikuwa cheo chake.
 
Alidai kuwa upande wa mashtaka, ulitengeneza barua hiyo baada ya kuona makosa waliyoyafanya hayatakidhi matakwa ya upande wa mashtaka na hivyo yatazua mapingamizi, na kwamba kwa kuzingatia hoja hiyo, wanaiomba mahakama barua hiyo isipokewe. 
 
Pili, Wakili Emanuel Safari alidai kuwa anapinga kupokewa kwa barua hiyo ya 8/8/2013 kama kielelezo cha upande wa mashtaka kwanza, kwa mujibu wa kumbukumbu zao katika kesi hiyo, shahidi huyo wa tisa, awali alidai mahakamani hapo alipewa maelekezo na SSP Ramadhan Ng’anzi ambaye ni RCO.
 
Alidai kuwa kutokana na utata wa cheo kilichotumika katika barua hiyo ya makabidhiano, ni wazi kwamba imetengenezwa na kutiwa saini na Ramadhan Ng’anzi (RCO) kwa kukimbiziwa siku mbili zilizopita, ambazo mahakama iliahirisha shauri hilo kutokana na kuugua ghafla kwa shahidi wa tisa.
 
Tatu, Wakili John Lundu alidai kuwa kielelezo hicho hakipaswi kupokelewa kwa sababu kimetengenezwa kwa ajili ya kukidhi matakwa ya sasa ya upande wa mashtaka, hivyo upande wa utetezi unaiomba mahakama hiyo isipokee barua hiyo kama kielelezo.
 
Baada ya muda mfupi, Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdalah Chavula alisimama na kuieleza mahakama kwamba hoja zilizotolewa na upande wa utetezi ni dhaifu na hazina mashiko ya kisheria na vile vile ni pre-mature.
 
Wakili huyo wa serikali, alidai kwamba uhalali wa kupokelewa kwa kielelezo ambacho ni nyaraka, kinapimwa na Sheria ya Ushahidi, Sura ya 6 ya Sheria iliyofanyiwa Marejeo mwaka 2002, kifungu cha 63, 64 na 66.
 
“Kwa mtizamo wa nyaraka hii, utagundua kwamba ni halisi, jambo ambalo inaifanya ikidhi vigezo nilivyovitaja katika vifungu vya 63, 64 na 66. Wenzetu (upande wa utetezi)hawakatai kwamba nyaraka hii ni halisi. Ukiitazama vizuri imesainiwa na SSP Ramadhan Ng’anzi na si ACP. Na hakuna kanuni au sheria inayomtaka mtu anaposaini barua kuweka cheo chake chini ya saini, huo ni utashi wa mtu binafsi.”alidai Wakili Chavula.
 
Wakili Chavula aliendelea kudai kuwa, ndani ya Comitto (siku ambayo mahakama kuu ilisomewa kwa mara ya kwanza kesi hiyo), nyaraka hiyo ilisomwa katika orodha ya vidhibiti ikiwamo barua hiyo ilitajwa.
 
Wakili Chavula alidai: “Ni makosa kuibua suala la Chain of Custody (mlolongo wa makabidhiano), wakati wa hatua ya kupokea kielelezo. Tunaomba tuielekeze mahakama dhidi ya shauri la Chalo Said Kibiru na mwenzake dhidi ya Jamhuri. Suala la ku-establish Chain of Custody ni endelevu, na kwa kuwa ni endelevu ni makosa ni makosa kuibua suala hili katika hatua ya kupokea kielelezo,”
Aliendelea kudai: Vile vile tunapenda tuielekeze mahakama yako tukufu katika sheria ifuatayo, Kifungu namba 245, kifungu kidogo cha 6, cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002.”
 
Kadhalika, alidai kwamba, kwa kuwa hoja zilizoibuliwa na upande wa utetezi zinagusa maudhui ya kielelezo hicho hata mahakama haijajua ni yapi, sheria inaelekeza kwamba maudhui ya nyaraka inayobishaniwa itajulikana baada ya kielelezo kupokelewa na mahakama, na hivyo upande wa mashtaka unaiomba mahakama kupokea kielelezo hicho na kupuuza hoja za utetezi.
 
Baada ya mabishano hayo ya kisheria kumalizika kati ya upande wa utetezi na upande wa mashtaka, Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo alitoa uamuzi na kumaliza mvutano huo, akisema mahakama hiyo imepokea barua hiyo kama kielelezo cha upande wa mashtakla baada ya kujiridhisha inakidhi vigezo vya kisheria.
 
Jaji Salma alipomaliza kutoa uamuzi huo, Wakili Chavula alisimama na kumwelekeza shahidi huyo wa tisa, kusoma kilichomo ndani ya barua hiyo ya makabidhiano mbele ya mahakama hiyo.
 
Shahidi huyo, aliisomea mahakama hiyo, barua ya makabidhiano hayo, yenye kumbukumbu namba KR/ CIA/ BI/ 22/ VOL. III ambayo iliandikwa Agosti 8, mwaka 2013.
 
CHANZO: NIPASHE.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa