Moshi. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi jana iliendelea kupokea vielelezo vinavyohusu tukio la mauaji ya Bilionea Erasto Msuya, aliyeuawa kwa kupigwa risasi wilayani Hai, Agosti mwaka jana.
Tangu kuanza kwa kesi hiyo, vielelezo karibu vyote ambavyo upande wa mashtaka umekuwa ukiomba vipokelewe vimekuwa vikipata pingamizi toka kwa mawakili wa utetezi.
Jana Jaji Salma Maghimbi anayesikiliza kesi hiyo alikubali kupokea barua ya makabidhiano ya vielelezo mbalimbali kutoka kwa shahidi wa tisa, Inspekta Samwel Maimu, licha ya mawakili wa utetezi kupinga.
Akipokea barua hiyo, Jaji Maghimbi alisema pamoja na mapingamizi hayo ya mawakili wa utetezi, mahakama inapokea barua hiyo, lakini hoja zao zitazingatiwa wakati wa kutoa maamuzi.
Kabla ya Jaji kupokea kielelezo hicho, Wakili wa Serikali, Abdallah Chavulla alimwongoza shahidi huyo kutoa ushahidi wake na mahojiano kati ya wakili huyo na shahidi yalikuwa kama ifuatavyo;
Wakili Chavulla: Shahidi hebu tukumbushe, tarehe 7.7.2013, ulifanya nini?
Shahidi: Nakumbuka siku hiyo nilikuwa eneo la tukio na nilikusanya vielelezo na kuchora ramani.
Wakili Chavulla: Ulikusanya vielelezo vipi?
Shahidi: Gari, risasi ya SMG, bastola ya marehemu, magazini mbili, simu mbili na tablet moja.
Wakili Chavulla: Baada ya kukusanya ulifanya nini?
Shahidi: Tulivikusanya kwenye bahasha vikiwa chini ya ulinzi wangu.
Wakili Chavulla: Kulikuwa na bahasha ngapi zilizotumika kuhifadhia vielelezo hivyo?
Shahidi: Kila kielelezo kilikuwa na bahasha yake.
Wakili Chavulla: Kwenye hizo magazini kulikuwa na risasi ngapi?
Shahidi: Magazini ndogo ilikuwa na risasi saba na nyingine ilikuwa na risasi 23.
Wakili Chavulla: Kipi kitakufanya utambue hizo bahasha ulizoweka vielelezo?
Shahidi: Bahasha zote nilikuwa nimeweka label (alama) niliandika exhibit (kielelezo) na namba ya kesi.
Wakili Chavulla: Unaweza ukaieleza mahakama namba ipi uliiweka?
Shahidi: Bomang’ombe yaani MB/IR/2786 ya mwaka 2013.
Wakili Chavulla: Tuambie uliendelea kukaa na hifadhi ya hivyo vielelezo mpaka lini?
Shahidi: Nilikaa navyo mpaka siku ya pili na nilitoa simu mbili na tablet moja nilimkabidhi Inspekta William kwa ajili ya uchunguzi, lakini alinirudishia ile tablet wakati ule ule.
Wakili Chavulla: Makabidhiano yenu mlifanya kwa njia ipi?
Shahidi : Tulifanya makabidhiano kwa njia ya barua.
Wakili Chavulla: Ukionyeshwa hiyo barua unaweza kuitambua?
Shahidi: Ndiyo
Wakili Chavulla: Nini kitakufanya uitambue hiyo barua?
Shahidi: Nitaweza kuitambua kwa sababu kuna sahihi yangu.
Wakili Chavulla: (akimpa barua ya makabidhiano) unaitambuaje hiyo barua?
Shahidi: Naitambua kwa sababu ina jina langu, sahihi yangu na namba yangu ya simu.
Wakili Chavulla: Ungependa itolewe kama kielelezo mahakamani?
Shahidi: Ndiyo ningependa.
Hata hivyo wakili wa utetezi John Lundu, Emmanuel Safari na Hudson Ndusyepo walipinga kupokewa kwa barua hiyo, akidai kwa dosari zilizopo inaonekana barua hiyo ilitengenezwa.
Wakili Ndusyepo alidai kutokana na mazingira ya kesi hiyo na hoja walizonazo upande wa utetezi, polisi hawakuzingatia sheria ya makabidhiano na wameitengeneza ili kukidhi matakwa yao.
Kwa mujibu wa Ndusyepo, barua hiyo inaonyesha imetengenezwa baada ya upande wa mashtaka kuona mazingira ya mapingamizi yao, dhidi ya vielelezo vilivyokusanywa na shahidi huyo.
Wakili huyo alidai Agosti 8, 2013 aliyekuwa RCO Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi hakuwa na cheo cha Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP) kama barua hiyo ya makabidhiano inavyoeleza.
Alifafanua kuwa wakati kesi hiyo inaanza, RCO huyo alijitambulisha kwa cheo cha Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), hivyo barua yenye cheo cha ACP ya mwaka 2013 ilitengenezwa.
Ni kutokana na mapungufu hayo, anaamini barua hiyo imetengenezwa baada ya kuona kesi hiyo mahakamani na baada ya kuona makosa waliyoyafanya, hivyo wakaomba barua isipokelewe.
Kwa upande wake, wakili Safari katika hoja zake alidai barua hiyo imetengenezwa kwa vile imesainiwa kwa cheo cha ACP, lakini ukiangalia maneno yaliyochapishwa yanaonesha cheo cha SSP.
Alisema kwa mujibu wa kumbukumbu walizopewa, shahidi huyo anaeleza alipewa maelekezo ya kwenda eneo la tukio na SSP, hivyo barua hiyo imetengenezwa kati ya Ijumaa na jana.
Wakili huyo alisema Jumatano iliyopita, shahidi alitoa ushahidi wake na kusema alipofika walikusanya vielelezo vyote na mpaka siku hiyo vilikuwa kwake, ambapo alitoa gari kama kielelezo na walikataa.
Naye Wakili Lundu alisema kuwa anaungana na mawakili wenzake, na kwamba ukiisoma hiyo barua utaona uongo umejileta katika sahihi ya aliyekuwa RCO Kilimanjaro.
Akijibu hoja hizo, wakili Chavula alisema hoja za mawakili hao ni dhaifu na hazina mashiko kisheria na ni wazi kinachobishaniwa ni sahihi na si maudhui ya barua.
Alisema vifungu vya 63,64 na 66 sura ya 6 mapitio ya sheria ya mwaka 2002, kielelezo hicho ni halisi, jambo ambalo linakifanya kikidhi mahitaji kutokana na vifungu vya kisheria vilivyotajwa.
Chavula alisema katika hoja za mawakili wenzake hawasemi kwamba ule waraka si halisi, ila wanasema wakati anasaini alikuwa na cheo cha SSP, lakini barua hiyo imesainiwa kwa cheo cha ACP.
Wakili Chavula alisema ukitazama barua hiyo, sahihi imekorogwa, huwezi ukajua maneno yaliyokuwa kwenye hiyo saini na huwezi kubaini alikuwa anamaanisha nini kwenye sahihi yake.
Alisema hakuna kanuni au sheria inayomtaka mtu anayesaini barua au nyaraka yeyote kumtaka kuweka cheo chake, na kwamba ni namna gani sahihi itawekwa ni utashi wa mtu binafsi.
Wakili huyo alisema mawakili wenzake wanachanganya mambo mawili kwa wakati mmoja, wanachanganya suala la ushahidi na uzito ambao ushahidi unatakiwa upewe na mahakama.
Alisisitiza kuwa hoja zilizoibuliwa mahakamani hapo na mawakili wa utetezi zinagusa maudhui ya kielelezo hicho, ambacho hata hivyo kilikuwa bado hakijapokelewa na mahakama.
Jaji Maghimbi alikipokea kielelezo hicho na kesi hiyo iliendelea kusikilizwa leo.
0 comments:
Post a Comment